Jul 19, 2016 07:40 UTC
  •  MONUSCO: Uganda na Congo zishirikiane kuwamaliza waasi

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umetoa wito wa kufanyika mashambulizi ya pamoja ya nchi za Uganda na Congo dhidi ya waasi The Allied Democratic Forces (ADF) wanaodhaniwa kufanya mauaji ya raia huko mashariki mwa Congo.

Naibu Kamanda wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Congo, Jenerali Jean Bao amesema kuwa, suala la wapiganaji wa kundi la The Allied Democratic Forces (ADF) na makundi mengi waitifaki wake nje ya Congo linaweza kutatuliwa kwa kushirikishwa washirika wa kigeni kama Uganda. Bao amesema lengo la kufanyika operesheni kama hiyo ni kuzuia usajili wa wanachama wapya, usafirishaji wa fedha na miamala mingine isiyo halali kati ya pande mbili za mpaka wa Congo na nchi nyingine husika. Jenerali huyo Mfaransa ameeleza masikitiko yake kutokana na kushindwa kulinda maisha ya watu wasio na hatia mbele ya jinai za kutisha za kundi hilo katika eneo la Beni huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Waasi wa kundi la The Allied Democratic Forces (ADF) wanatuhumiwa kuua zaidi ya raia 600 katika eneo la Beni.

Tags