Namibia: Hatutoruhusu meli ya silaha za Israel kutia nanga nchini kwetu
Meli ya MV Kathrin iliyokuwa ikisafiri kutoka Vietnam imenyimwa kibali cha kutia nanga katika Bandari ya Walvis, pwani ya Namibia, huku Waziri wa Sheria wa Namibia akisema kuwa nchi yake inafungamana na wajibu wa kutounga mkono au kuhusika katika uhalifu wa kivita wa Israel.
Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Namibia imeizuia meli ya MV Kathrin iliyokuwa ikisafiri kutoka Vietnam kutia nanga katika Walvis Bay.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, Waziri wa Sheria wa Namibia anasisitiza kuwa nchi yake inaheshimu wajibu wa kutounga mkono au kuhusika katika uhalifu wa kivita wa Israel.
Katika taarifa yake, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeipongeza Namibia kwa kuzuia kutia nanga meli hiyo iliyokuwa imebeba silaha kwa ajili ya kupelekewa utawala ghasibu wa Kizayuni.
Namibia imekuwa ikiliunga mkono taifa la Palestina. Ikumbukwe kuwa, mwaka 2021, Namibia ilikuwa miongoni mwa mataifa ya Kiafrika yaliyolalamikia vikali kitendo cha kuruhusiwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika (AU).
Serikali ya Windhoek inasisitiza kuwa, kuudhinisha utawala haramu kuwa mwanachama wa mtazamaji wa AU kunakinzana moja kwa moja na malengo na thamani za umoja huo wa kibara.