Rais Pezeshkian: Wairani wameungana kuilinda nchi yao dhidi ya vitisho
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139088-rais_pezeshkian_wairani_wameungana_kuilinda_nchi_yao_dhidi_ya_vitisho
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kwamba taifa litalinda uhuru na mamlaka yake ya kitaifa licha ya kuongezeka vitisho na mashinikizo.
(last modified 2026-06-12T12:48:20+00:00 )
Jun 12, 2026 12:44 UTC
  • Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian
    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kwamba taifa litalinda uhuru na mamlaka yake ya kitaifa licha ya kuongezeka vitisho na mashinikizo.

Akihutubia Mkutano Mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Tiba cha Iran mapema leo Ijumaa mjini Tehran, Pezeshkian ameashiria duru mbili za vita dhidi ya Iran katika mwaka mmoja—vita vya siku 12 mnamo Juni 2025 na uchokozi unaoendelea sasa wa Marekani na Israel, ulioanza Februari 28—na kusisitiza kwamba vitendo vya uhasama ni njama za wazi za kutaka kusimamisha maendeleo ya Iran.

"Licha ya mashinikizo na vitisho vyote, taifa la Iran litatetea uhuru, hadhi, ardhi na mamlaka yake ya kujitawala," amesema Rais Pezeshkian.

Matamshi hayo yametolewa siku moja baada ya Rais wa Marekani kutishia kuipiga Iran kuipiga "VIKALI SANA Iran USIKU WA LEO" na kuvamia kisiwa cha kimkakati cha Kharg nchini Iran, kabla ya kurudi nyuma saa chache baadaye na kudai kwamba makubaliano kati ya Tehran na Washington yanakaribia.

Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba umoja na mshikamano wa kitaifa ndiyo mtaji muhimu zaidi wa Iran katika mazingira ya sasa.

Rais Pezeshkian amesema kuwa umma umeonyesha nia yake thabiti ya kutetea maslahi ya taifa. Ametaja mikutano ya hadhara inayoendelea nyakati za usiku kote nchini Iran, akisema kwamba uwepo endelevu wa taifa katika medani na nyanja mbalimbali "umezuia njama za maadui" na kuvuruga mahesabu yao.

Kwa zaidi ya usiku 100, raia wa Iran wamekuwa wakikusanyika katika mitaa ya miji mikubwa, kuonesha uungaji mkono wao kwa Jamhuri ya Kiislamu na majeshi ya taifa yanayopambana na adui katika medani za vita.