Sudan: RSF inafanya biashara haramu ya viungo vya binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139148-sudan_rsf_inafanya_biashara_haramu_ya_viungo_vya_binadamu
Serikali ya Sudan imelituhumu kundi la Rapid Support Forces (RSF) kuwa linaendesha mtandao wa biashara haramu ya viungo vya binadamu ndani ya magereza ya Daqris na Shala huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, ambalo kwa mujibu wa makadirio ya serikali ya Khartoum, lina wafungwa karibu 20,000 wa kijeshi na raia.
(last modified 2026-06-15T04:27:01+00:00 )
Jun 15, 2026 04:24 UTC
  • Kinara wa RSF Hamdan Dagalo akiwahutubia wapiganaji wake
    Kinara wa RSF Hamdan Dagalo akiwahutubia wapiganaji wake

Serikali ya Sudan imelituhumu kundi la Rapid Support Forces (RSF) kuwa linaendesha mtandao wa biashara haramu ya viungo vya binadamu ndani ya magereza ya Daqris na Shala huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, ambalo kwa mujibu wa makadirio ya serikali ya Khartoum, lina wafungwa karibu 20,000 wa kijeshi na raia.

Hata hivyo afisa mmoja katika ofisi ya vyombo vya habari ya RSF amekanusha tuhuma hizo.

Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Al-Harith Idris, amelituhumu kundi hilo kuwa linaendesha mtandao wa biashara ya viungo vya binadamu ndani ya magereza katika barua aliyoituma kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Rais wa Baraza la Usalama Leonor Zalapata Torres.

Kwa mujibu wa barua hiyo, serikali ya Sudan imesema ina ripoti zinazofichua kuwepo mtandao wa biashara haramu ya viungo vya binadamu katika gereza la Dagris, unaohusisha pia wafanyakazi wa matibabu wa kigeni wanaoshukiwa kuwa na uraia wa Colombia na Serbia.

Barua hiyo imesema, wahanga wa biashara hiyo kutoka jeshi, vikosi vya pamoja vya Harakati ya Darfur na raia wanahamishwa kwa kisingizio cha kuachiliwa huru, na baadaye wanakabidhiwa kwa maafisa wa kigeni huko Nyala ili kunyofoa viungo vyao, na kisha maiti zao zinazikwa katika makao makuu ya Kitengo cha 16 cha RSF "ili kufuta ushahidi."

Barua ya mjumbe huyo wa Sudan UN inaonyesha kwamba kuna wafungwa 19,800 wanaoshikiliwa na RSF katika gereza la Daqris huko Nyala, wakiwemo wanajeshi 3,795 wa jeshi la Sudan, maafisa wa polisi 4,270, na raia wapatao 10,500, wakiwemo mamia ya wanawake.

Imefichua kwamba wafungwa katika gereza la Daqris wanasumbuliwa na mateso na unyanyasaji wa kimfumo, ikiwa ni pamoja na kuteswa kwa nyaya za umeme, huku kukiwa na ripoti za uhaba mkubwa wa chakula na maji ya kunywa, kusambaa magonjwa na kunyimwa matibabu.

Kwa mujibu wa takwimu zilizojumuishwa katika barua hiyo, hali hiyo katika gereza la Daghris husababisha vifo vya zaidi ya wafungwa 4 kila wiki kutokana na njaa, magonjwa na kuenea kwa magonjwa, hasa kipindupindu.

Katika gereza la Shala, ambalo linadhibitiwa na RSF tangu Oktoba 2025, barua iliyotumwa kwa Umoja wa Mataifa imefichua kuwa waasi hao wanawashikilia wanajeshi 881, raia 407 na makumi ya watoto chini ya umri wa miaka 18.

Barua hiyo inasema kwamba wafungwa wa kiraia wamepata majeraha makubwa na kuvunjika mifupa kutokana na shambulio la RSF huko El Fasher, na kwamba makumi ya wafungwa wameaga dunia kutokana na kuvunda majeraha yao na ukosefu wa huduma za matibabu.

Kwa upande mwingine, barua hiyo imeeleza kwamba RSF huacha miili ya marehemu gerezani kwa muda mrefu na kuwalazimisha wafungwa kuwazika wenzao wenyewe katika ua wa magharibi, mita 400 kutoka gerezani.