Burundi yaomba msaada huku watu 193 wakilazwa hospitalini kwa maradhi ya Mpox
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115782-burundi_yaomba_msaada_huku_watu_193_wakilazwa_hospitalini_kwa_maradhi_ya_mpox
Wizara ya Afya ya Umma ya Burundi imesema watu 193 wamelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa Mpox huku ikihamasisha umma kukomesha kuenea kwa ugonjwa huo.
(last modified 2024-08-29T08:22:01+00:00 )
Aug 29, 2024 08:22 UTC
  • Burundi yaomba msaada huku watu 193 wakilazwa hospitalini kwa maradhi ya Mpox

Wizara ya Afya ya Umma ya Burundi imesema watu 193 wamelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa Mpox huku ikihamasisha umma kukomesha kuenea kwa ugonjwa huo.

Wizara hiyo imesema katika taarifa kuwa watu 231 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo kufikia Agosti 25 na kati ya wagonjwa hao 38 wametibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani. Hakuna kifo kimoja kilichoripotiwa.

Kati ya visa 231 vilivyoripotiwa,  wagonjwa 136 wanatoka wilaya za Bujumbura Kaskazini, Kayanza na Bujumbura Kusini.

Wilaya 29 kati ya 49 nchini zimeripoti angalau kisa kimoja chanya cha Mpox.

Burundi, taifa la kipato cha chini linalohangaika na ufadhili wa afya ya umma, halina vifaa vya kutosha vya afya na wafanyakazi wanashughulikia dharura hiyo ya afya ya umma kwa kuhamasisha watu juu ya hatua za kuuzuia, haswa katika maeneo ya umma kama vile soko, makanisa na shule.

Bujumbura, mji mkuu wa kibiashara, ambako visa vingi vinaripotiwa, haina maji safi ya kutosha wala vifaa vya usafi, suala ambalo kwa kiasi fulani limelaumiwa kueneza ugonjwa huo.

Wakati huo huo wakala wa Afya wa Umoja wa Afrika jana ulieleza kuwa unakaribia kupata karibu dozi milioni moja za chanjo ya mpox, na kuwataka wazalishaji kuzipatia taasisi nyingine teknolojia ya kutengeneza chanjo ya mpox ili kukabiliana na ugonjwa huo.

Katika hali ambayo Afrika iko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mpox, Shirika la Afya Duniani (WHO) mapema mwezi huu lilitangaza dharura ya kimataifa kutokana na kuenea kwa ugonjwa huo wa virusi.

Jeann Kaseya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) ameliambia kongamano la kikanda la WHO lililofanyika katika Jamhuri ya Kongo kuwa bara la Afrika linaelekea kupata karibu dozi milioni moja za mpox.