Wairani 24,000 wameingia Saudia kwa ajili ya ibada ya Hija
Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara la Iran amesema kuwa takribani Wairani 24,000 tayari wamewasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija mwaka huu, ambapo kati yao takribani 14,000 wako Makka, na zaidi ya 10,000 wapo Madina.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, likinukuu tovuti rasmi ya Hija, Alireza Rashidian, amesema Wairani waliofika Saudia tayari wanaendelea kutekeleza ibada mbali mbali wakisuburi kuanza rasmi Ibada ya Hija. Amebainisha kuwa wote waliofika Saudia wapo katika hali njema ya kiafya na mazingira yao kwa ujumla ni mazuri.
Wakati huo huo, huku mamilioni ya Waislamu wakitarajiwa kuhudhuria ibada ya Hija mwaka huu, vikosi vya usalama vya Saudi Arabia vimeimarisha hatua za kukabiliana na watu wanaojaribu kuingia Makkah na maeneo matakatifu bila vibali rasmi vya Hija.
Vyombo vya usalama vinaendelea na juhudi za kuzuia watu wasiokuwa na vibali vya Hija kuingia au kukaa katika mji wa Makkah na maeneo matakatifu, vikionya kwamba wanaokiuka sheria hizo pamoja na wanaowasaidia watakamatwa na kukabiliwa na hatua za kisheria.
Kabla ya kuanza kwa msimu wa Hija, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia ilitangaza faini zinazokadiriwa kati ya riyali 20,000 hadi 100,000 za Saudi (takribani dola 5,330 hadi 26,660) kwa yeyote atakayekiuka kanuni za Hija.
Wizara hiyo imesisitiza wito wake kwa raia, wakazi na wenye visa kufuata kikamilifu kanuni za Hija na kuepuka adhabu za kisheria, ikikumbusha kuwa kupata kibali halali cha Hija ni sharti la lazima.