Hizbullah yafanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya Israel Kusini mwa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i138304-hizbullah_yafanya_mashambulizi_dhidi_ya_vikosi_vya_israel_kusini_mwa_lebanon
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema imefanya operesheni 20 za kijeshi dhidi ya vikosi vamizi vya Israel katika maeneo ya kusini mwa Lebanon, huku mapigano yakiendelea licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoongezwa hadi katikati ya mwezi Mei.
(last modified 2026-05-12T09:08:59+00:00 )
May 12, 2026 09:07 UTC
  • Hizbullah yafanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya Israel Kusini mwa Lebanon

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesema imefanya operesheni 20 za kijeshi dhidi ya vikosi vamizi vya Israel katika maeneo ya kusini mwa Lebanon, huku mapigano yakiendelea licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoongezwa hadi katikati ya mwezi Mei.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu usiku, Hizbullah ilisema wapiganaji wake walilenga mikusanyiko ya wanajeshi wa Israel pamoja na magari ya kijeshi katika maeneo ya al-Bayyadah, Rishaf na Tayr Harfa kwa kutumia makombora, mizinga na ndege zisizo na rubani zenye milipuko.

Hizbullah imesema katika operesheni hizo liliharibu kifaru aina ya Merkava mjini Rishaf pamoja na magari kadhaa ya kijeshi ya uhandisi, gari la kivita aina ya Hummer, na tingatinga za kijeshi za D9 karibu na Naqoura na barabara ya al-Bayyadah.

Katika mji wa Taybe, Hizbullah imesema imefanya mashambulizi ya hatua kadhaa kwa kutumia ndege tatu zisizo na rubani zilizolenga nyumba iliyokuwa ikitumiwa na wanajeshi wa Israel. Kundi hilo limesema kuwa mashambulizi hayo yalisababisha majeruhi waliolazimisha uhamishaji wa waliojeruhiwa kwa helikopta.

Mashambulizi mengine yaliripotiwa kulenga maeneo yenye wanajeshi wa Israel karibu na mto Deir Siriane pamoja na vituo vipya vya amri na mizinga katika maeneo ya Odaisseh na al-Bayyadah.

Hizbullah pia imesema kuwa vikosi vyake vya ulinzi wa anga vilidungua ndege ya kijasusi ya Israel juu ya eneo la Tyre kwa kutumia kombora la ardhini kwenda angani.

Mapigano hayo yanaendelea huku Israel ikiwa bado inakalia kwa mabavu eneo la ukanda wa kusini mwa Lebanon linaloingia kati ya kilomita tano hadi kumi ndani ya ardhi ya Lebanon. Jeshi la Israel limeendelea kuwaonya wakazi wa kusini mwa Lebanon kutorejea katika maeneo hayo.

Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza Aprili 17 na kuongezwa hadi katikati ya Mei, mashambulizi ya kila siku yameendelea kuripotiwa nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon, mashambulizi ya Israel tangu Machi 2 yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 2,869 na kuwafanya zaidi ya watu milioni moja kuyahama makazi yao.