Kesi za Mpox Nigeria zafika 48, zimeenea katika mji mkuu, majimbo 20
Kesi za ugonjwa wa Mpox nchini Nigeria zimeongezeka hadi 48, huku virusi hivyo sasa vikiripotiwa katika mji mkuu Abuja na majimbo mengine 20.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC), licha ya kuongezeka visa hivyo, lakini hakuna vifo vilivyoripotiwa kutokana na ugonjwa huo hadi sasa.
Siku ya Jumatano Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa Nigeria imepokea dozi 10,000 za chanjo ya Mpox, na kuwa nchi ya kwanza katika kanda ya Afrika kupokea chanjo hiyo.
Umoja wa Afrika umetangaza dharura ya afya ya umma ili kukabiliana na kuenea kwa kasi kwa virusi katika bara zima.
Mpox ni ugonjwa wa virusi ambao umeathiri nchi nyingi na kusababisha kutangazwa hali ya dharura ya afya ya umma ya kimataifa.
Mpox huenezwa zaidi na mguso wa moja kwa moja kutoka kwa mnyama mgonjwa, akiwa na au bila dalili, hadi kwa mtu mwenye afya. Pia kuna maambukizi kutoka kwa mtu mgonjwa hadi kwa mtu mwenye afya. Pia hupitishwa kutoka kwa mama mgonjwa hadi kwa mtoto wake wakati wa ujauzito
Dalili huonekana siku 5 hadi 21 baada ya kuambukizwa na hujumuisha homa, maumivu ya mwili, nodi za lymph zilizovimba na vidonda vya ngozi. Ingawa hakuna matibabu maalumu, dawa za kuzuia virusi zinaweza kusaidia kudhibiti hali hiyo. Kesi nyingi ni nyepesi na ahueni hutokea ndani ya wiki chache.