WHO: Chanjo za mpox kuwasili hivi karibuni DRC
Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa shehena ya kwanza ya chanjo ya virusi vya homa ya nyani (mpox) inatarajiwa kuwasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika siku chache zijazo.
Hayo yameelezwa na mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus baada ya kurejea siku ya Ijumaa kutoka nchini Kongo huku akisema kuwa katika siku zijazo chanjo zaidi zitawasilishwa nchini humo.
Agosti 14 mwaka huu, WHO ilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa virusi vya mpox, hasa kuongezeka kwa visa vya maambukizi vya aina mpya ya virusi hivyo inayofahamika kama Clade 1b nchini Kongo na katika nchi jirani.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani - WHO, karibu visa 15,000 vya mpox vimegundulika nchini Kongo katika mwaka wa 2024, huku kukiwa na vifo 500.
Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema anaamini kuwa maambukizi ya virusi vya homa ya nyani, yanaweza kutokomezwa ndani ya miezi sita ijayo.
Ghebreyesus amesema licha ya kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache. Licha ya kauli yake, hadi sasa bara la Afrika lenye maambukizi mengi zaidi limepokea kiasi kidogo cha chanjo dhidi ya mpox.