Miili 22 ya wahajiri yapatikana katika Pwani ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11689-miili_22_ya_wahajiri_yapatikana_katika_pwani_ya_libya
Miili 22 ya wahajiri imepatikana ndani ya boti karibu na pwani ya Libya katika Bahari ya Mediterranean huku juhudi za kutafuta miili zaidi zikiendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2016 09:09 UTC
  • Miili 22 ya wahajiri yapatikana katika Pwani ya Libya

Miili 22 ya wahajiri imepatikana ndani ya boti karibu na pwani ya Libya katika Bahari ya Mediterranean huku juhudi za kutafuta miili zaidi zikiendelea.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF limesema miili hiyo ilipatikana jana Jumatano karibu na pwani ya Libya na kwamba timu za waokoaji na wapiga mbizi zimeokoa manusura zaidi ya 200 wa ajali hiyo ya kutatanisha. Taarifa ya MSF imeongeza kuwa, miili 21 kati ya 22 iliyopatikana ni ya wanawake na maiti moja ni ya mwanaume. Jens Pagotto, ofisa wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, watoto wadogo 50 ni miongoni mwa 200 waliookolewa.

Mapema mwezi huu, miili zaidi ya 200 ya wahajiri ilipatikana katika mabaki ya boti iliyozama katika Bahari ya Mediterranean Aprili mwaka jana 2015, kusini mashariki mwa Italia, yapata kilomita 135 kaskazini mwa Libya. Hivi karibuni, Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilisema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya, kusini mwa Italia.

Baadhi ya wahajiri wakijaribu kuokoa maisha yao

 

Wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine zaidi ya 3,000 wakifariki dunia kwa kuzama baharini.