Nigeria kuandamana leo kupinga ongezeko la gharama za maisha
(last modified Tue, 01 Oct 2024 02:18:21 GMT )
Oct 01, 2024 02:18 UTC
  • Nigeria kuandamana leo kupinga ongezeko la gharama za maisha

Wananchi wa Nigeria leo Jumanne wamepanga kufanya maandamano mapya kulalamikia ongezeko la gharama za maisha. Maandamano hayo yaliyopewa jina la "Oktoba Mosi Bila Hofu" yamepangwa kwenda sambamba na kumbukumbu ya maadhimisho ya miaka 64 ya uhuru wa Nigeria.

Waratibu wa maandamano hayo wamesema kuwa yatafanyika katika mji mkuu Abuja, katika mji wa bandari wa Lagos na katika makao makuu ya majimbo ya Nigeria. 

Maandamano sawa na hayo yaliyopangwa kufanyika leo yaliitikisa Nigeria mwezi Julai na Agosti mwaka huu wakati waandamanaji walipotaka kurejeshwa kwa ruzuku ya mafuta na kukomeshwa ufisadi serikalini. 

Wanaharakati wa Nigeria wamesema kuwa, karibu watu 12 waliuawa katika maandamano hayo wakati wa makabiliano na polisi. 

Katika siku yake ya kwanza mamlakani, Rais Bola Tinubu wa Nigeria alihitimisha ruzuku ya mafuta iliyodumu kwa miongo kadhaa nchini humo ambayo ilisaidia pakubwa kupunguza bei za bidhaa muhimu za mahitajio. Serikali yake pia ilipunguza mara mbili thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kusababisha bei ya karibu kila kitu kupanda.

Rais Bola Tinubu wa Nigeria 

Licha ya Rais Tinubu kutetea sera zake katika hotuba yake kwa taifa lakini alishindwa kufikia muafaka na wafanyamaandamano.