Bunge la Kenya lamtimua Naibu Rais, Rigathi Gachagua
(last modified Wed, 09 Oct 2024 03:43:51 GMT )
Oct 09, 2024 03:43 UTC
  • Bunge la Kenya lamtimua Naibu Rais, Rigathi Gachagua

Bunge la Kitaifa la Kenya limepasisha kwa wingi wa kura hoja ya kumng’oa madarakani Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua.

Wabunge 281 kati ya 349 walipiga kura Jumanne jioni kumtimua naibu huyo wa Rais William Ruto, miaka miwili tu tangu waingie madarakani baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge 44 walipiga kura kupinga hoja hiyo huku mmoja akijizuia kupiga kura, na hivyo hoja hiyo ikapasishwa na zaidi ya thuluthi mbili ya kura zilizohitajika.

Gachagua anakabiliwa na msururu wa tuhuma zikiwemo za ufisadi, kukiuka katiba, kumhujumu rais na kushajiisha migawanyiko ya kikabila. Gachagua anakuwa Naibu Rais wa kwanza kuvuliwa mamlaka na Bunge chini ya Katiba ya 2010.

Seneti itaunda Kamati Maalum ya Wanachama 11 kuchunguza madai hayo ndani ya muda wa siku saba. Baadaye Kamati hiyo itaripoti matokeo yake kwa Seneti ndani ya siku 10.

Bunge la Kitaifa la Kenya

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira pia ataalikwa kufika yeye binafsi au kuwakilishwa mbele ya kamati maalum ya Seneti wakati wa uchunguzi dhidi yake, ambapo baraza hilo litatoa uamuzi wake.

Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse aliwasilisha mashtaka 11 yaliyojumuisha ulimbikizaji wa mali ya Shilingi bilioni 5.2 za Kenya kupitia njia za ufisadi katika miaka miwili akiwa naibu rais pamoja na madai ya kuwagawanya Wakenya kwa kauli yake kwamba serikali ya Kenya Kwanza imeundwa na ‘wenye hisa’ pekee.