Watu milioni 1.9 waathiriwa na mafuriko Chad huku mikoa yote 23 ikiathiriwa
(last modified Sun, 13 Oct 2024 02:12:06 GMT )
Oct 13, 2024 02:12 UTC
  • Watu  milioni 1.9  waathiriwa na mafuriko Chad huku mikoa yote 23 ikiathiriwa

Mikoa yote 23 ya Chad imeathiriwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini humo.

Zaidi ya watu 550 wamefariki dunia na nyumba 210,000 zimesombwa na maji. Msimu wa mvua kubwa  kwa  kawaida huendelea hadi mwezi  Oktoba.

Takriban hekari 432,000 za ardhi na mifugo 72,000 zimeharibiwa. Haya yanajiri huku nchi hiyo ikitangaza dharura ya usalama wa chakula na lishe mwezi Februari uliopita.

Kati ya takriban watu milioni 1.9 walioathirika nchini humo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) linasema wanawake 85,000 wanakadiriwa kuwa wajawazito.

Familia sasa zimejificha kwenye mabanda na katika maeneo ya shule, kuachwa bila kupata huduma za afya, maji safi ya kunywa, vyoo safi, na kwamba magonjwa  ya  kuhara, malaria, magonjwa ya kupumua na ya  ngozi yanaweza kuongezeka.

UNFPA imesema iko tayari kusaidia Wizara ya Afya ya Umma na Kinga kutoa huduma za afya ya uzazi na ulinzi na vifaa vya usafi kwa waathirika hao. Baadhi ya wakunga 248 wametumwa kutoa huduma za afya ya uzazi huko Chad.

Hatari za kiusalama vile vile  zimeongezeka sana dhidi ya wanawake na wasichana katika mabanda hayo ya muda, ambapo hawana maeneo ya  faragha hata  kidogo, na wakati wanapotoka nje kutafuta chakula na kuni katika mazingira hatarishi na yasiyo salama hukumbwa na changamoto nyingi.

Mafuriko makubwa katika Ukanda wa Afrika Magharibi na Kati yamesababisha mgogoro kwa karibu watu milioni mbili.

Tags