Maelfu ya raia wa Sudan Kusini wakimbilia Uganda
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, maelfu ya raia wa Sudan Kusini wamekimbilia katika nchi jirani ya Uganda.
Ripoti ya UNHCR inaonyesha kuwa, takribani raia elfu kumi wa Sudan Kusini wameingia nchini Uganda na kuomba hifadhi katika nchi hiyo. Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR akthari ya raia hao wa Sudan Kusini wanaoingia nchini Uganda wanataabika na tatizo la njaa na lishe duni. Kuanzia Julai 7 mwezi huu mji mkuu Juba ulianza kushuhudia mapigano ya umwagaji damu baina ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomtii Riek Machar ambaye ni Makamu wa Rais.
Hadi sasa watu wasiopungua 300 wameripotiwa kuuawa katika sokomoko na mapigano hayo. Tangu yalipoibuka mapigano hayo hadi sasa takribani raia 18 elfu hadi elfu 20 wameikimbia nchi hiyo na kuelekea katika nchi jirani ya Uganda.
Duru za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nazo zinaripoti kwamba, maelfu ya wakimbizi wa Sudan Kusini wameingia katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo katika siku za hivi karibuni. Mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu yanasema kuwa, wakimbizi walioko katika vijiji vya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanakabiliwa na hali duni ya kimaisha. Serikali ya Kinshasa imelitaka Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kuchukua hatua za maana za kuwafikishia misaada ya kibinadamu wakimbizi hao pamoja na raia wa nchi hiyo walioko katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amekataa kuheshimu makataa ya masaa 48 aliyopewa na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo awe amerejea katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba.
Siku ya Alkhamisi, Rais Salva Kiir alimpa makamu wake masaa 48 awe amerejea mjini Juba kwa kile alichosema kuwa, kuendeleza utekelezaji wa makubaliano ya amani. Kadhalika Rais Salva Kiir aliahidi kudhamini usalama wa Machar wakati wa kurejea kwake mjini Juba. Machar alitoweka mjini Juba tangu yaliposhadidi mapigano kati ya wanajeshi wanaomuunga mkono na wale wa Rais Kiir mjini hapo.
Riek Machar alikabidhiwa tena wadhifa wa Makamu wa Rais kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka jana.
Baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa Sudan Kusini, wananchi wa nchi hiyo walipata matumaini ya kufikia tamati vita vya miaka miwili katika nchi yao. Hata hivyo wakati wananchi hao wakijiandaa kuadhimisha miaka mitano tangu nchi yao ijitenge na Sudan na kujitangazia uhuru na mamalaka ya kujitawala yaani Julai 9, kwa mara nyingine tena Sudan Kusini ilitumbukia katika mapigano ya umwagaji damu.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuendelea mapigano hayo ni tishio kubwa kwa mkataba wa amani ambao pande mbili ziliahidi kufungamana nao kwa ajili ya kurejesha amani na kuandaa mazingira mwafaka kwa ajili ya kuikarabati tena nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe.