Wabeba silaha waua wanakijiji 15 katika jimbo la Benue, Nigeria
(last modified Fri, 01 Nov 2024 09:39:01 GMT )
Nov 01, 2024 09:39 UTC
  • Wabeba silaha waua wanakijiji 15 katika jimbo la Benue, Nigeria

Kwa akali watu 15 wameuawa katika shambulizi la 'majambazi' waliojizatiti kwa silaha katika jimbo la Benue katikati mwa Nigeria.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo leo Ijumaa na kueleza kuwa, watu kadhaa pia wamejeruhiwa wakati majambazi hao walipovamia kitongoji kimoja kilichoko katika mji wa Anyiin, eneo la Logo jimboni Benue.

Bado haijafahamika ni kundi gani lililohusika na shambulio hilo la umwagaji damu la jana Alkhamisi. Hata hivyo jimbo la Benue ni sehemu ya ukanda wa kati wa Nigeria ambako makundi ya uhalifu yanatumia mashambulizi ya silaha baada ya miaka kadhaa ya machafuko ya kijamii kati ya wafugaji na wakulima. 

Mapigano makali kati ya wafugaji wa kabila la Fulani wanaohamahama na wakulima, wakizozania ardhi, maeneo ya kulishia mifugo na maji kwa miaka kadhaa sasa yameyaathiri maeneo ya katikati mwa Nigeria.  

Magenge ya wabeba silaha Nigeria

Kwa muda mrefu sasa, Nigeria imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya magenge yenye silaha pamoja na hujuma za kundi la kigaidi la Boko Haram na lile la Daesh (ISIS) tawi la Afrika Magharibi (ISWAP) katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo.

Licha ya hukumu ya kifo kutekelezwa kwa wanaopatikana na hatia ya utekaji nyara, lakini matukio ya utekaji kwa ajili ya kudai fidia yameshadidi katika maeneo hayo.