RSF yaendeleza hujuma za umwagaji damu Sudan
Kwa akali watu 18 wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa katika mashambulizi mawili tofauti ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa, watu 15 waliuawa na watano kujeruhiwa katika shambulio la RSF jana Jumamosi kwenye eneo la Bardik na vijiji vya karibu.
Huku hayo yakiarifiwa, Ibrahim Khatir, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya jimbo la Darfur Kaskazini ameiambia Xinhua kwamba, watu watatu waliuawa katika shambulio jingine la mizinga kwenye Hospitali ya Saudi huko El Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini.
Habari zaidi zinasema kuwa, wafanyakazi wa huduma za matibabu katika hospitali hiyo hawakujeruhiwa katika hujuma hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres siku ya Ijumaa alilaani mashambulizi ya karibuni dhidi ya raia yaliyofanywa na wapiganaji wa RSF.
Mzozo unaoendelea kutokota nchini Sudan, ulioanza katikati ya Aprili 2023, umesababisha vifo vya zaidi ya watu 24,850, na mamilioni ya watu kuyahama makazi yao, kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya mashirika ya kimataifa.