Jeshi latumwa mitaani kuzima ghasia za baada ya uchaguzi Msumbiji
(last modified Sat, 09 Nov 2024 03:19:40 GMT )
Nov 09, 2024 03:19 UTC
  • Jeshi latumwa mitaani kuzima ghasia za baada ya uchaguzi Msumbiji

Msumbiji imetuma wanajeshi mitaani kusaidia kudumisha utulivu kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya ghasia dhidi ya chama tawala ambacho kinatuhumiwa kwa udanganyifu katika uchaguzi wa mwezi uliopita.

Msemaji wa jeshi la Msumbiji Jenerali Omar Saranga ametoa tangazo hilo na kuongeza kuwa, "Katika nyakati kama hizi, huku maandamano yakifanyika katika baadhi ya mikoa, tuna jukumu la kuunga mkono vikosi vya usalama katika kudumisha utulivu na amani ya umma."

Hospitali kubwa zaidi ya Msumbiji ilisema jana Ijumaa kuwa, watu wasiopungua watatu waliuawa na 66 kujeruhiwa wakati wa makabiliano baina ya polisi na waandamanaji wanaolalamikia matokeo ya uchaguzi wenye utata.

Volker Turk, Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka mvutano na machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Msumbiji ambayo yameshapelekea watu 20 kupoteza maisha huku usalama ukizidi kudorora. Hata hivyo takwimu za Kituo cha Demokrasia na Haki za Kibinadamu cha Msumbiji zinaonyesha kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika ghasia hizo wanapindukia 34.

Machafuko ya baada ya uchaguzi yachachamaa nchini Msumbiji

Ghasia hizo ziliikumba katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baada ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kuwa, Daniel Chapo wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) ameshinda kwa asilimia 70 ya kura, lakini wapinzani wamekataa kutambua matokeo hayo. Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye kwa mujibu wa tume hiyo ameshika nafasi ya pili kwa asilimia 20.32 ya kura ameendelea kutoa mwito wa kupinga matokeo hayo akiyataja kuwa ni ya udanganyifu.

Baraza la Katiba la nchi hiyo halijapasisha na kubariki matokeo ya uchaguzi ili kukiidhinisha rasmi na kisheria chama tawala kurefusha uongozi wake wa karibu miongo 5.