Raila Odinga kuhuisha ndoto ya kuunganisha nchi za Afrika
(last modified Mon, 11 Nov 2024 06:08:29 GMT )
Nov 11, 2024 06:08 UTC
  • Raila Odinga kuhuisha ndoto ya kuunganisha nchi za Afrika

Fikra ya waziri mkuu wa zamani wa Kenya ya kutaka kuziunganisha pamoja nchi za Afrika imemulikwa na kuakisiwa katika vyombo mbalimbali vya habari vya kikanda na kimataida.

Duru mbalimbali za habari za kikanda zimeripoti kuwa, fikra ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, ya kuunganisha nchi za Afrika inafanana na aliyekuwa ya Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi aliyeuawa katika machafuko ya mwaka 2011 na makundi ya wanamgambo yaliyokuwa yakisaidiwa na nchi za magharibi chini ya mwavuli wa Shirika la Kijeshi la Nchi za magharibi (NATO).

Gaddafi aliwahi kupigia debe wazo la kubuniwa ‘Muungano wa Mataifa ya Afrika’ (United States of Africa) ili kuimarisha uchumi na umoja wa bara hilo.

MSiku ya Ijumaa iliyopita, Bw Odinga akiwa Addis Ababa, Ethiopia, alitilia mkazo haja ya umoja wakati huu anapowania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

 “Nina maono makubwa kwa Afrika; bara lenye umoja, mshikamano, utajiri na amani,” alisema Raila Odinga.

Alisisitiza kuwa: “Umoja wa Afrika ni muhimu sana kwangu. Lazima turejeshe umoja ili uwe kipaumbele kama walivyofanya Mwalimu Nyerere na Nkrumah.”

Julai 1999, Muammar Gaddafi alihimiza suala la kuawepo mshikamano zaidi baina ya mataifa ya Afrika katika masuala ya siasa na uchumi alipohutubia Kongamano la Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

 Gaddafi alisema: “Lazima tubuni bunge na benki ya Afrika. Bunge hili litapiga jeki azma ya bara kuungana huku benki ikiharakisha utekelezaji wa mikataba ya kuunda jumuiya ya kiuchumi Afrika.

Mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, Raila Odinga, alitangaza rasmi kuwa atagombea uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika anahudumu kwa muda wa miaka minne ambao unaweza kuongezewa muda mara moja.