Kuanzia Italia hadi Japan, watu wote wanaichukia Israel
(last modified Thu, 05 Jun 2025 13:00:08 GMT )
Jun 05, 2025 13:00 UTC
  • Kuanzia Italia hadi Japan, watu wote wanaichukia Israel

Mitazamo hasira na ya ghadhabu dhidi ya Israel inaendelea kuongezeka duniani kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza. Chuki na hasira hizo dhidi ya Israel zinaongezeka hata katika nchi ambazo kwa jadi zinauunga mkono kwa nguvu utawala wa Kizayuni, kama vile Hungary na Poland.

Idadi kubwa ya watu duniani wana mtazamo hasi na wa hasira kuhusu Israel na waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu.

Matokeo ya kura ya maoni ya taasisi ya Pew yaliyotolewa hivi karibuni kabisa yanaonesha kuwa, wimbi la chuki na hasira dhidi ya Israel linaongezeka duniani na halizuiliki.

Tangu zamani watu wengi katika nchi za Kiarabu na Kiislamu wamekuwa na mtazamo hasi na mbaya kuhusu Israel tena kwa miongo mingi, lakini uchunguzi wa maoni wa taasisi ya Pew unaonesha kuongezeka sana mitazamo hasi kote barani Ulaya na Asia Mashariki. Pia unaonesha kuwa maoni chanya kuhusu Israel yanapungua kwa kasi katika nchi za Ulaya Magharibi hususan miongoni mwa vijana.

Nchini Italia, asilimia 66 ya watu walioulizwa walikuwa na maoni hasi kuhusu Israel. Huko Ugiriki, Sweden na Uhispania pia, maoni hasi dhidi ya Israel yamedhihirika kuwa juu ya asilimia 70. Nchini Uholanzi, idadi ya watu wanaoichukia Israel kutokana na jinai zake imefikia asilimia 78.

Hata katika nchi kama Poland, ambayo serikali yake kijadi inaiunga mkono Israel, maoni ya umma yalikuwa mabaya kwa asilimia 62. Kadhalika, huko Hungary, asilimia 53 ya waliohojiwa imedhihirika wana mitazamo hasi na ya hasira kuhusu Israel.

Uchunguzi wa maoni wa taasisi ya Pew pia umeonesha kuongezeka hisia hasi dhidi ya Israel nchini Indonesia, nchi yenye Waislamu wengi zaidi duniani, ambapo asilimia 80 ya waliohojiwa wanaiona Israel ni adui wa ubinadamu.

Kwingineko barani Asia, maoni yalikuwa mabaya. Asilimia 80 ya waliohojiwa nchini Japan na asilimia 60 ya nchini Korea Kusini wote wana mtazamo hasi na mbaya kuhusu Israel kutokana na jinai zake za kutisha huko Palestina na hasa Ghaza.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, Wamarekani wengi, asilimia 53, wana maoni mabaya kuhusu Israel. Idadi hiyo imeongezeka kutoka asilimia 42 mwezi Machi 2022, kabla ya shambulio la Octoba 7, 2023 hadi mwezi Aprili mwaka huu wa 2025. Uchunguzi wa maoni wa taasisi ya Pew umegundua kuwa, wengi wa Wamarekani wana maoni yasiyowapendeza Wazayuni kuhusu Israel.

Chuki dhidi ya nduli wa Ghaza, Benjamin Netanyahu pia zimeongezeka sana. Huko Australia, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki, Indonesia, Italia, Japan, Uholanzi, Uhispania, Uswidi (Sweden) na Uturuki, karibu robo tatu ya watu wazima hawana imani kabisa na Netanyahu na wanamchukia sana.