Iran, Imarati zasisitiza haja ya Waislamu kote duniani kuwa na umoja
(last modified Sat, 07 Jun 2025 07:00:23 GMT )
Jun 07, 2025 07:00 UTC
  • Iran, Imarati zasisitiza haja ya Waislamu kote duniani kuwa na umoja

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran na Kiongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan wametoa wito wa umoja wa Waislamu.

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa, umoja na mshikamano miongoni mwa nchi zote katika ulimwengu wa Kiislamu ndiyo suluhu ya changamoto zinazoukabili umma huo.

Pezeshkian aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan jana Ijumaa, kwa mnasaba wa Idd al-Adh'ha, mojawapo ya sikukuu muhimu zaidi katika kalenda ya Kiislamu.

Rais wa Iran ameeleza matumaini yake kuwa sherehe hiyo adhimu ya Kiislamu itatayarisha uwanja wa kuendeleza amani, kutokomeza vita na ukosefu wa usalama katika eneo na kuanzishwa kwa amani na usalama endelevu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ameitaja Idd al-Adh'ha kuwa ni dhihirisho la wazi la mshikamano, umoja na mshikamano baina ya Waislamu duniani kote kwa kuzingatia kanuni za Uislamu na Qur’ani Tukufu, mafundisho ya Mtume Muhammad (saw) na Kibla cha pamoja.

Dakta Pezeshkian amewatakia kheri na fanaka wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu, UEA na mataifa yote ya Kiislamu duniani.

Rais wa Imarati kwa upande wake ametoa pongezi zake kwa serikali na taifa la Iran kwa mnasaba wa sikukuu ya Idd al-Adh'ha na kueleza matumaini yake kuwa, maadhimisho haya yatawakurubisha zaidi Waislamu na kuimarish mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu.