Wafanyakazi wa bandari Ufaransa, Italia wazuia kupelekwa silaha Israel
(last modified Sat, 07 Jun 2025 06:58:17 GMT )
Jun 07, 2025 06:58 UTC
  • Wafanyakazi wa bandari Ufaransa, Italia wazuia kupelekwa silaha Israel

Wafanyakazi wa bandari za Ufaransa na Italia wameendelea kufanya mgomo wao na kukataa kupakia shehena za silaha na zana za kijeshi zinazopelekwa Israel, wakisema kuwa hawatahusika katika "mauaji ya halaiki" yanayoendelea Gaza.

Vyombo vya uchunguzi vya Ufaransa na Ireland vimefichua kwamba, meli ya mizigo ya ZIM Contship Era, iliratibiwa kupita kwenye bandari ya Fos-sur-Mer ya Marseille ili kupakia kwa siri tani 14 za suhula za kijeshi zilizotengenezwa na kampuni ya Ufaransa ya Eurolinks.

Ilikusudiwa kufika katika bandari za Genoa na Salerno nchini Italia kabla ya kuelekea katika Bandari ya Haifa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Hiyo ni shehena ya tatu ya aina hiyo kutoka Marseille hadi Israel mwaka huu 2025, kufuatia usafirihaji kama huo Aprili 3 na Mei 22, zote zikihusisha silaha za kijeshi zinazotumika kurefusha muda wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Katika taarifa iliyotolewa Juni 2, Muungano Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi (CGT), unaowakilisha wafanyakazi wa bandari katika Ghuba ya Fos, ulitangaza kuwa, "Bandari ya Marseille-Fos haipasi kutumika kusambazia silaha jeshi la Israel."

Taarifa hiyo imesema, "Mahamali na wafanyakazi wengine wa bandari hawatashiriki katika mauaji ya kimbari yanayoendelea. Tunasimamia amani na tunapinga vita vyote vinavyoleta vifo, mashaka na watu kuhama makazi yao."

Mitazamo hasira na ya ghadhabu dhidi ya Israel inaendelea kuongezeka duniani kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza. Matokeo ya kura ya maoni ya taasisi ya Pew yaliyotolewa hivi karibuni kabisa yanaonesha kuwa, wimbi la chuki na hasira dhidi ya Israel linaongezeka duniani na hususan katika nchi za Ulaya, na halizuiliki. Nchini Italia, asilimia 66 ya watu walioulizwa walikuwa na maoni hasi kuhusu Israel. Huko Ugiriki, Sweden na Uhispania pia, maoni hasi dhidi ya Israel yamedhihirika kuwa juu ya asilimia 70. Nchini Uholanzi, idadi ya watu wanaoichukia Israel kutokana na jinai zake imefikia asilimia 78.