Wahamiaji 604 walizuiwa kuendelea na safari kwenye pwani ya Libya wiki iliyopita
(last modified Tue, 19 Nov 2024 11:10:05 GMT )
Nov 19, 2024 11:10 UTC
  • Wahamiaji 604 walizuiwa kuendelea na safari kwenye pwani ya Libya wiki iliyopita

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa, wahamiaji 604 walikamatwa na kurudishwa nje ya pwani ya Libya wiki moja iliyopita wakati walipokuwa wanahatarisha maisha yao kujaribu kuelekea barani Ulaya kwa kutumia vyombo dhaifu mno vya baharini.

IOM imesema katika taarifa yake kwamba, wahamiaji waliokamatwa kati ya Novemba 10 hadi 16 ni pamoja na wanawake 34 na watoto 11 na kuongeza kuwa, miili saba ya wahamiaji imepatikana huku wengine 54 hawajulikani walipo hadi hivi sasa na kuna uwezekano mkubwa nao wamekufa maji.

Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, wahamiaji 20,231 wamezuiwa kuendelea na safari, huku 515 wakifariki na wengine 830 kutoweka kwenye pwani ya Libya.

Ardhi ya Libya inatumiwa sana na wahamiaji haramu wanaojaribu kuelekea barani Ulaya

 

Mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, shirika hilo la kimataifa la uhamiaji lilitangaza kwamba, wahamiaji 979 walikuwa wameokolewa na kurudishwa nchini Libya katika kipindi cha wiki moja.

Sehemu moja ya taarifa ya IOM ilisema: "Kuanzia tarehe 25 hadi 31 Agosti 2024, wahamiaji 979 walizuiwa kuendelea na safari za hatari na kurudishwa Libya.

Tangu ilipopinduliwa serikali ya kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi mwaka 2011 hadi hivi sasa, ukosefu wa usalama na machafuko yaliyofuatia nchini Libya yamesababisha wahamiaji wengi, haswa kutoka nchi za Afrika za kusini mwa jangwa la Sahara kutuumia ardhi ya nchi hiyo kujaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea barani Ulaya.