Mapigano yashadidi huko El Fashe, Sennar yapokea raia wanaorejea makwao
(last modified Wed, 27 Nov 2024 03:12:27 GMT )
Nov 27, 2024 03:12 UTC
  • Mapigano yashadidi huko El Fashe, Sennar yapokea raia wanaorejea makwao

Mji wa El Fasher, magharibi mwa Sudan, umeshuhudia mapigano kati ya jeshi na Vikosi vya kundi la Msaada wa Haraka (RSF), huku raia wakianza safari ya kurejea makwao katika Jimbo la Sennar kusini mashariki mwa nchi hiyo baada ya jeshi kulidhibiti eneo hilo.

Ripoti zinasema kuwa, mapigano ya silaha nyepesi na za kati yalitokea Jumanne asubuhi kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa RSF mashariki mwa mji huo.

Ripoti zinasema kuwa ndege za jeshi la Sudan mapema jana zilishambulia kwa mabomu ngome za Vikosi vya Msaada wa Haraka kaskazini, mashariki na kusini mwa mji wa El Fasher.

Kwa upande mwingine, vyanzo vya Sudan vimethibitishia kwamba raia wa vijiji vingi katika Jimbo la Sennar wameanza kurejea makwao baada ya jeshi la serikali kulidhibiti tena eneo hilo.

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha wananchi wakisherehekea kurejea katika makazi yao katika maeneo ya Kirkuk, Al-Dindar na Al-Suki, huku jeshi likianza kutoa huduma za kibinadamu katika maeneo hayo yaliyokuwa yakisumbuliwa na kukatika maji na umeme baada ya uporaji uliofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.