Rais wa Comoro aazimia kumkabidhi mwanawe madaraka
Rais wa Comoro, Azali Assoumani kwa mara ya kwanza amesema hadharani kuwa ana nia ya kukabidhi madaraka kwa mwanawe Nour El Fath atakapoondoka madarakani mwaka wa 2029; na kuthibitisha tetesi za wakosoaji wake kwamba amekuwa akimtayarisha kwa muda mrefu mwanawe kumrithi.
Assoumani, ambaye kuchaguliwa kwake tena mwaka mmoja uliopita kulikumbwa na madai ya wizi wa kura, alimteua El Fath kuwa msimamizi wa kuratibu masuala ya serikali, na kumpa pia mamlaka makubwa juu ya baraza la mawaziri. Assoumani aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1999 kupitia mapinduzi, na ameshinda chaguzi nne tangu 2002.
Akizungumzia muda wake wa kuondoka madarakani utakapofika, Assoumani amesema katika hotuba yake kwa wafuasi wa kisiwa cha Moheli kwamba, "Nitamsimika mwanangu kuchukua nafasi yangu kama mkuu wa serikali na chama."
Chama tawala kinachoongozwa na Assoumani kilishinda uchaguzi wa bunge mwezi huu, ingawa vyama vya upinzani vilisusia zoezi hilo, huku vingine vikipinga matokeo yake kwa madai kuwa kulikuwa na udanganyifu.

Nour El Fath Azali aliye na umri wa miaka 39, alishinda kiti cha uwakilishi bungeni kuliwakilisha eneo bunge nje kidogo ya mji mkuu Moroni. Amekuwa mshauri binafsi wa babake, Rais Azali Assoumani.
Azali Assoumani alichaguliwa tena kuwa Rais wa visiwa vya Comoro Januari mwaka jana baada ya kushinda uchaguzi uliopingwa na vyama vya upinzani na kuibua maandamano makubwa ya siku mbili visiwani humo.