Mapigano yashadidi DRC huku waasi wa M23 wakisonga mbele kuelekea Goma
Mapigano kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kundi la waasi la M23 yanaripotiwa kushadidi huku waasi hao wakisonga mbele kuelekea Goma mashariki mwa nchi hiyo.
Ripoti zinaeleza kuwa, wasiwasi mkubwa umeibuka katika mji wa Goma huku idadi ya wakimbizii ikiongozeka.
Mapigano kati ya jeshi la Congo na waasi yamezusha mzozo wa kibinadamu huku juhudi za kidiplomasia kupatanisha mvutano kati ya viongozi wa Congo na Rwanda zimeshindwa.
Tangu mazungumzo ya amani kushindikana, wapiganaji wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na wanajeshi wa Rwanda wameteka maeneo mengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika wiki za hivi karibuni, na kusababisha mgogoro wa kibinadamu kuukumba mji mkuu wa jimbo hilo, ambao ni makazi ya watu wapatao milioni mbili.
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mzozo unaoendelea katika jimbo la Kivu Kaskazini umesababisha maelfu kwa maelfu ya watu kuyahama makazi mwaka huu na huenda ukazua vita vya kikanda.
Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Matthew Saltmarsh, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba idadi ya waliokimbia makazi yao kufikia sasa ni zaidi ya watu 400,000 mwaka huu pekee, hii ikiwa karibu mara mbili ya idadi iliyoripotiwa wiki iliyopita.
Huku mapigano yakizidi, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, umesema kwamba vikosi vyake vya kulinda amani, vilishiriki katika mapigano makali dhidi ya M23.