Maharusi 1,000 kutoka mataifa 43 ya Afrika wajumuika pamoja nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121990-maharusi_1_000_kutoka_mataifa_43_ya_afrika_wajumuika_pamoja_nchini_ethiopia
Zaidi ya maharusi na wanandoa 1,000 kutoka mataifa 43 tofauti ya Afrika walijumuika pamoja Jumapili kushiriki katika sherehe ya harusi ya kiutamaduni na hilo ni tukio la kwanza la aina yake katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
(last modified 2025-01-27T23:27:31+00:00 )
Jan 27, 2025 23:27 UTC
  • Maharusi 1,000 kutoka mataifa 43 ya Afrika wajumuika pamoja nchini Ethiopia

Zaidi ya maharusi na wanandoa 1,000 kutoka mataifa 43 tofauti ya Afrika walijumuika pamoja Jumapili kushiriki katika sherehe ya harusi ya kiutamaduni na hilo ni tukio la kwanza la aina yake katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Masharika mbalimbali ya habari yaliakisi habari hiyo jana ikiwemo hii taarifa inayosema kwamba, baada ya kupata habari ya kuweko hafla hiyo ya kihistoria ya harusi ya halaiki katika mji mkuu wa Ethiopita, Addis Ababa, Henry Kinda na mchumba wake Roth Kinda waliamua kushiriki kwa hamu kwenye uzoefu huo wa ajabu na wa kipekee. 

Mara tu baada ya matayarisho yao kukamilika bwana na bibi harusi  hao wamesafiri kutoka Msumbiji hadi Ethiopia. Huko wameungana na zaidi ya wanandoa 1,000 kwenye sherehe hiyo ya kiutamaduni.

Hafla hiyo imewajumuisha pamoja wanandoa kutoka mataifa 43 ya Afrika, ikiwemo mwenyeji wao Ethiopia, na kila mmoja kwa utamaduni wake, waliweza kuoanisha tamaduni tofauti za Kiafrika katika hafla hiyo ya kihistoria.

Mabwana na mabibi harusi kwenye sherehe za "Harusi ya Maelfu" nchini Ethiopia

 

Jina ya hafla hiyo lilikuwa ni "Harusi ya Maelfu" na kaulimbiu ilikuwa ni "Kuunda Familia ni Sawa na Kujenga Taifa." Harusi hiyo ya umati ilikuwa na mila na desturi za kila namna yakiwemo matambiko yaliyokita mizizi katika tamaduni za Ethiopia na za Kiafrika.

Wanandoa na familia zao, wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni, waliimeremetesha shughuli hiyo na kuifanya kuwa sherehe ya kupendeza iliyooanisha tamaduni tofauti na kuonesha pia urithi tajiri wa nchi za Afrika.

Wanandoa walipata pia fursa ya kupokea ushauri nasaha na mafunzo ya stadi za maisha pamoja na uzoefu wa kona mbalimbali za bara la Afrika, kutoka kwa makungwi na watu waliobobea katika stadi za maisha ya ndoa.