UN yaelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka ghasia DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121996-un_yaelezea_wasiwasi_wake_kuhusu_kuongezeka_ghasia_drc
Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa kutokana na kuongezeka ghasia na mapigano ya silaha huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
(last modified 2025-01-27T23:33:39+00:00 )
Jan 27, 2025 23:33 UTC
  • UN yaelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka ghasia DRC

Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa kutokana na kuongezeka ghasia na mapigano ya silaha huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizunguumza kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya amesema: "Hali inazidi kuzorota kwa kasi."

Amesema mamia ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameuawa au kujeruhiwa katika wiki chache zilizopita na mamia ya maelfu wamekimbia nyumba na makazi yao ili kukwepa kudhuriwa na risasi na makombora.

Mapigano yamekuwa yakiongezeka kati ya Jeshi la Serikali na waasi wa M23 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Waasi waliuteka mji wa Sake na ambao ndio ulikuwa mji wa mwisho muhimu kuweko mikononi mwa serikali kabla ya Goma, makao makuu ya Kivu Kaskazini. Goma ndicho kitovu na miji ya mashariki mwa DRC.

Naye Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Operesheni za Amani amesema kuwa, Umoja wa Mataifa unasikitishwa sana na kuanza tena mapigano ambayo yamesababisha kupotea fursa ya kimkakati ya kutatua mgogoro wa DRC.

Kwa upande wake, Stephane Dujarric, msemaji mkuu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema kuwa, Guterres "anasikitishwa sana na kuongezeka ghasia mashariki mwa DRC." Guterres ametoa mwito wa kusitishwa mapigano mara moja. Zaidi ya watu 400,000 wamekimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa 2025 huko mashariki mwa DRC.