Waislamu wa Uganda wamtaka Museveni aunde Wizara ya Masuala ya Waislamu
Waislamu nchini Uganda wameitaka serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni wa nchi hiyo iunde wizara maalumu ya kushughulikia masuala ya Waislamu.
Sheikh Magid Bagalaaliwo, Mkuu wa Kamati ya Hazina ya Zaka nchini Uganda amemtaka Rais Museveni aunde Wizara ya Masuala ya Waislamu ambayo itakuwa na jukumu la kushughulikia masuala ya Waislamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mkuu wa Kamati ya Hazina ya Zaka nchini Uganda amesema kuwa, wameshawasilisha ombi lao hilo kwa Rais Museveni hata hivyo bado hawajapata jibu.
Aidha Mkuu wa Kamati ya Hazina ya Zaka nchini Uganda amekosoa utendaji wa serikali ya uganda na kusema kuwa, idadi ya Waislamu wenye nyadhifa mbalimbali serikali hususan katika baraza la mawaziri ni ndogo mno.
Ameongeza kuwa, hata wale Waislamu ambao wamepewa nyadhifa serikali sio nafasi muhimu. Kiongozi mwingine wa Waislamu nchini Uganda amesema kuwa, kuna Waislamu milioni kumi wanaoishi nchini Uganda hivyo kuna haja ya kutengwa wizara maalumu ya kushughulikia masuala ya wafuasi wa dini hiyo tukufu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waislamu wa Uganda wamekuwa wakilalamikia vikali mauaji yanayofanywa mara kwa mara dhidi ya masheikh na viongozi wa Kiislamu nchini humo.
Baadhi ya viongozi wa Kiislamu nchini Uganda wanalituhumu jeshi la polisi nchini humo kwamba, halijawajibika vyema katika kushughulikia mauaji yanayofanywa dhidi ya masheikh katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mara kadhaa Mufti wa Uganda Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje ameitaka serikali na mashirika ya usalama ya nchi hiyo yanayochunguza mauaji ya viongozi wa Kiislamu kufanya kazi kiuadilifu na kwa viwango vya juu vya utaalamu.