Mashirika ya misaada Sudan Kusini yaitaka UN kuwasaidi walioathiriwa na vita
Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanayohudumu Sudan Kusini yameutaka Umoja wa Mataifa uandae uwanja mzuri wa kuwasaidia raia walioathiriwa na vita vya ndani nchini humo.
Mashirika hayo yanayolijumisha Shirika la Oxfam na Kamati ya Kimataifa ya Uokovu yametoa taarifa ya pamoja kufuatia kuchapishwa ripoti kuhusu kushindwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kuwalinda raia wa Sudan Kusini mbele ya mashambulizi ya vikosi vya jeshi la serikali, vikiwemo vitendo vya kuwabaka wanawake.
Kikosi cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini kina wanajeshi karibu elfu 12 ambao wana mamlaka ya kuwakabili wanamgambo wenye silaha ili kuwalinda raia wa nchi hiyo.
Kikosi hicho pia kina jukumu la kudhamini usalama wa misaada ya kibinadamu inayopelekwa kwa raia wa Sudan Kusini.
Raia wa Sudan Kusini karibu milioni nne na laki nane ambao ni takribani nusu ya jamii yote ya nchi hiyo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.