'Baba wa Taifa' wa Namibia aaga dunia akiwa na miaka 95
Rais wa kwanza wa Namibia huru, Sam Nujoma, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 katika mji mkuu wa nchi hiyo, Windhoek.
Rais wa sasa wa nchi hiyo, Nangola Mbumba ametangaza hayo na kuongeza kuwa, Nujoma alikuwa amelazwa hospitalini kwa muda wa wiki tatu zilizopita kutokana na ugonjwa ambao "hakuweza kupona".
Rais Mbumba amesema kifo cha muasisi huyo wa taifa huru la Namibia kilichotokea jana Jumamosi ni msiba mkubwa ambao umelitikisa taifa zima.
Nujoma aliongoza vita vya muda mrefu vya kudai uhuru kutoka kwa Afrika Kusini mwaka 1990 baada ya kusaidia kupatikana kwa vuguvugu la ukombozi la Namibia lililojulikana kama South West Peoples' Organization (Swapo) miaka ya 1960. Baada ya uhuru, Nujoma alikua rais mwaka 1990 na aliongoza nchi hadi 2005.
Nujoma alistaafu kama mkuu wa nchi mwaka 2005 lakini aliendelea kukiongoza chama hicho kabla ya kung'atuka mwaka 2007 kama rais wa chama tawala cha Swapo baada ya kukiongoza kwa miaka 47.
Sam Nujuma alifahamika zaidi kama "baba wa taifa" na kinara wa mapambano ya ukombozi wa Namibia, na alipendwa sana ndani na nje ya nchi. Namibia ilikuwa chini ya ukoloni wa Wajerumani kutoka 1884 hadi 1915, wakati Ujerumani ilipoteza koloni lake hilo katika Vita vya Kwanza vya Dunia.