Bunge la Libya lalaani njama za Wazayuni za kuwahamisha watu wa Ghaza
(last modified Sun, 09 Feb 2025 10:37:04 GMT )
Feb 09, 2025 10:37 UTC
  • Bunge la Libya lalaani njama za Wazayuni za kuwahamisha watu wa Ghaza

Bunge la Libya limelaani na kupinga njama za Marekani na Israel za kutaka kuwahamisha wananchi wa Ghaza na kuwapeleka sehemu nyingine nje ya ardhi zao za jadi za Palestina.

Katika taarifa yao wabunge wa Libya wamelaani vikali jaribio lolote la kuwahamisha wakazi wa Ghaza na njama yoyote ya kubadilisha muundo wa wakaazi wa ukanda huo na kusema kuwa huko ni kukanyaga waziwazi haki za Wapalestina.

Katika taarifa yao, wabunge wa Libya wamesema kuwa, wanafuatilia kwa karibu kauli na njama zote zinazolenga kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa, kauli na njama hizo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na haki za binadamu na ni uhalifu wa kivita unaokinzana na misingi yote ya kimataifa.

Vile vile Wabunge wa Libya wamesisitiza kuwa, utatuzi wa haki na wa kudumu la kadhia ya Palestina ni kukomesha uvamizi wa Israel na kuanzishwa taifa huru la Palestina ambalo mji mkuu wake ni Baytul Muqaddas kama yanavyosema maazimio halali ya kimataifa. Pia wametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa na taasisi za kikanda na kimataifa kutekeleza vilivyo majukumu yao ya kisheria na kimaadili ya kukomesha jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.

Aidha Wabunge wa Libya wamesisitizia mshikamano wao kamili na wananchi wa Palestina katika hatua hii muhimu wakisema kwamba, msimamo thabiti wa Libya katika kuunga mkono Muqawama wa wananchi wa Palestina ni jambo la wazi lisilotetereka kabisa.