Algeria yalaani matamshi ya kijuba ya Netanyahu kuhusu Wapalestina
Algeria imepinga kwa maneno makali matamshi ya kijuba ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliyetaka Wapalestina wapewe makazi mapya nje ya nchi yao na kwamba eti serikali ya Saudi Arabia imege ardhi yake na kuwapa Wapalestina waunde nchi yao.
Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imelaani matamshi hayo na kusema ni ya kejeli, ya kukera na kuchukiza mno.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Algiers inasisitiza kwa mara nyingine kuhusu wajibu wa kuheshimiwa haki ya kujitwala mipaka yote ya ardhi ya Saudi Arabia na itakuwa bega kwa bega na Riyadh mbele ya jaribio lolote la kudhoofisha mamlaka yake na umoja wa ardhi yake.
Taarifa ya wizara hiyo pia imetilia mkazo dhamira ya muda mrefu ya Algeria ya kutetea haki za Wapalestina na kukataa pendekezo lolote linalohatarisha mamlaka ya Palestina au umoja wa ardhi za mataifa ya Kiarabu.
Siku ya Alkhamisi, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, alitoa matamshi ya kijuba kwa kusema kuwa, Saudi Arabia ina maeneo mengi na rasilimali nyingi za ardhi, inaweza kumega sehemu ya ardhi yake na kuwapa Wapalestina ili waunde nchi yao.
Tangu wakati huo hadi hivi sasa, Netanyahu analaaniwa takriban kila siku. Mataifa mengi duniani yamejitokeza kulaani matamshi yake hayo na hasa hatua yake ya kudharau haki ya kujitawala ardhi ya nchi huru ambayo mipaka yake inatambuliwa rasmi kimataifa.
Watu wa mataifa mbalimbali wanasema kuwa, matamshi kama hayo hayawezi kumwepusha Netanyahu na kitanzi cha kesi ya mauaji ya kimbari na jinai za kivita na ataendelea kuandamwa na mahakama za kimataifa kwa uhalifu wake huo mkubwa wa kivita.