Nchi tatu za Afrika zasaini mkataba wa bomba la gesi asilia
Imeelezwa kuwa, nchi tatu za Afrika za Nigeria, Algeria na Niger zimefanikiwa kutiliana saini mkataba muhimu wa bomba la gesi asilia
Maafisa kutoka mataifa ya Algeria, Nigeria na Niger wametia saini mikataba mipya inayolenga kuharakisha uendelezaji wa mradi wa bomba kubwa la gesi asilia kuelekea barani Ulaya.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, maafisa kutoka Algeria, Nigeria na Niger wametiliana saini mikataba mipya ambayo kwa mujibu wake itaharakisha uendelezaji wa bomba kubwa la gesi asilia kuelekea katika mataifa ya Ulaya.
Bomba hilo la gesi lililotangazwa mwaka 2009, litasafirisha mabilioni ya mita za ujazo za gesi kutoka Nigeria kupitia Niger hadi Algeria.
Aidha kutoka hapo gesi hiyo itaweza kusafirishwa kupitia bomba la chini ya bahari kwenda nchini Italia, au kupakiwa kwenye meli za gesi asilia zilizowekwa kimiminika kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.
Nchi hizo tatu zilitia saini mikataba kuhusu ripoti ya upembuzi yakinifu na masuala mengine, ikiwa ni pamoja na makubaliano nyeti kati ya makampuni ya nishati ya serikali.
Mradi huo umepewa msukumo kutokana na ongezeko la mahitaji ya gesi na kupanda kwa bei ulimwenguni kote kufuatia vita vya Russia na Ukraine huku kukiwa na tishio dhidi ya nishati hiyo hususan barani Ulaya.