Mwenyekiti wa AU: Umoja wa Afrika wathamini uungaji Mkono wa Russia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139718-mwenyekiti_wa_au_umoja_wa_afrika_wathamini_uungaji_mkono_wa_russia
Umoja wa Afrika (AU) unathamini kwa dhati uungaji mkono wa Russia katika kushughulikia masuala muhimu ya bara la Afrika ndani ya baraza la Umoja wa Mataifa, na unakaribisha msimamo wa Moscow katika kuimarisha ufadhili wa vikosi vya kulinda amani barani Afrika.
(last modified 2026-07-08T04:46:53+00:00 )
Jul 08, 2026 04:44 UTC
  • Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC),  Mahmoud Ali Youssouf, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov
    Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC),  Mahmoud Ali Youssouf, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov

Umoja wa Afrika (AU) unathamini kwa dhati uungaji mkono wa Russia katika kushughulikia masuala muhimu ya bara la Afrika ndani ya baraza la Umoja wa Mataifa, na unakaribisha msimamo wa Moscow katika kuimarisha ufadhili wa vikosi vya kulinda amani barani Afrika.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC),  Mahmoud Ali Youssouf, siku ya Jumanne katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia (Urusi) , Sergey Lavrov, jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Youssouf amesisitiza kuwa: “Umoja wa Afrika pia unathamini msimamo wa Russia kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na uungaji mkono wake kwa matakwa halali ya Afrika ya kupata viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama, pamoja na viti vitano vya muda.”

Kwa upande wake, Lavrov amebainisha kuwa Russia na AU zimekubaliana kuimarisha uratibu ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kushikilia msimamo wa pamoja kuwa uwakilishi wa Afrika lazima uongezwe. Waziri huyo alisisitiza kuwa kuongeza uwakilishi wa Afrika kutasaidia kusahihisha dhuluma za kihistoria. Amesisitiza kuwa upanuzi wowote wa baadaye wa baraza hilo unapaswa kwanza kuwanufaisha mataifa ya Afrika badala ya madola ya Magharibi, ambayo alisema tayari yamejilimbikizia nguvu kubwa kupita kiasi.

Lavrov ameongeza kuwa Russia itaendelea kuwezesha utatuzi wa migogoro barani Afrika. Amesisitiza kuwa: “Wale wanaotaka kwa dhati kuwasaidia Waafrika kutatua migogoro mingi, ambayo mingi ilirithishwa kutoka enzi za ukoloni, wanapaswa kuwasaidia Waafrika kutekeleza mbinu za Kiafrika katika kutatua matatizo ya Kiafrika.”

Waziri huyo wa Russia amesisitiza kuunga mkono ajenda ya AU ya kudai fidia kutoka kwa wakoloni wa zamani.

Bwana Youssouf ameishukuru Russia kwa kusaidia mwitikio wa Afrika dhidi ya milipuko ya hivi karibuni ya Ebola, ikiwemo kwa kutoa vifaa vya kupima (PCR tests) na misaada ya kitabibu.

Lavrov amebainisha kuwa Moscow inatarajia Youssouf atashiriki katika Mkutano wa Tatu wa Russia-Afrika, utakaofanyika mwezi Oktoba.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia aliwasili Ethiopia siku ya Jumatatu ikiwa ni sehemu ya ziara yake barani Afrika. Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Lavrov nchini humo tangu mwaka 2022.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa moja ya mada kuu za mazungumzo wakati wa mikutano ya Lavrov inatarajiwa kuwa ujenzi wa kituo kikubwa cha nishati ya nyuklia katika taifa hilo la Afrika Mashariki, mradi unaoashiria hatua muhimu katika maendeleo ya kistratijia na uhuru wa nishati kwa taifa hilo.