Congo yaishtaki Rwanda katika Mahakama ya Afrika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imewasilisha kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ICJ kwa madai ya ukiukwaji wa haki.
Tuhuma za Congo dhidi ya Rwanda zinahusiana na mzozo uliokumba eneo la mashariki mwa nchi hiyo tangu 2021, ambako vikosi vyake vimekuwa vikabiliana na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda. Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani mwaka 2023 lakini itaanza kusikilizwa rasmi hapo kesho Jumatano ambapo hoja za pande hizo mbili kuhusu mamlaka ya mahakama hiyo na uwezo wake wa kusikiliza ombi iliyowasilishwa na DRC itasikilizwa.
Haya yanajiri siku chache baada ya Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, na Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC, kukutana jijini Dar es Salaam Tanzania, kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo yenye makao yake mjini Arusha Tanzania, Congo DR inadai kuwa mzozo huo umesababisha mauaji, uvamizi wa maeneo yake, na watu 520,000 kulazimika kuyahama makazi yao, kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu na uharibifu wa shule na hivyo kusababisha watoto 20,000 kukosa elimu.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aidha inalalamikia uharibifu wa miundombinu mbinu yake kama vile vifaa vya kusambaza umeme, uporaji na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na vituo vya afya.
Pia inadai kuwa Rwanda inawahifadhi watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa, na ambao mahakama zake zimetoa hati za kimataifa za kukamatwa kwao.