UNHCR: Tulihudumia makumi ya maelfu ya wakimbizi mwaka 2024 nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122746-unhcr_tulihudumia_makumi_ya_maelfu_ya_wakimbizi_mwaka_2024_nchini_libya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema kwenye ripoti yake ya karibuni kabisa kwamba, mwaka uliopita wa 2024 lilihudumia makumi ya maelfu ya wakimbizi nchini Libya pekee ikiwa ni pamoja na kuwarejesha makwao mamia ya wengine.
(last modified 2025-02-14T23:11:57+00:00 )
Feb 14, 2025 23:11 UTC
  • UNHCR: Tulihudumia makumi ya maelfu ya wakimbizi mwaka 2024 nchini Libya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema kwenye ripoti yake ya karibuni kabisa kwamba, mwaka uliopita wa 2024 lilihudumia makumi ya maelfu ya wakimbizi nchini Libya pekee ikiwa ni pamoja na kuwarejesha makwao mamia ya wengine.

Katika taarifa yake hiyo, UNHCR imesema: Mwaka 2024, makumi ya maelfu ya wakimbizi walipewa misaada ya matibabu, kifedha na vitu muhimu na shirika letu. Taarifa hiyo pia imesema wakimbizi 1,500 walihamishwa kutoka maeneo mbalimbali ya Libya na kupewa makazi mapya mwaka 2024.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: "Mwaka 2024 ... UNHCR ilitoa msaada wa kuokoa maisha na utatuzi wa muda mrefu kwa baadhi ya wakimbizi waliokuwa kwenye hatari zaidi."

"Wakimbizi 1,500 walihamishwa na kupelekwa maeneo salama, ili kuwapa nafasi ya kujenga upya maisha yao," imeongeza taarifa hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo fupi ya UNHCR, mwaka jana makumi ya maelfu ya wakimbizi nchini Libya wengi wao wakiwa ni kutoka nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara walipewa msaada wa matibabu na kifedha pamoja na vitu muhimu vya kujikimu katika maisha yao.

Libya imekumbwa na ukosefu mkubwa wa usalama na machafuko tangu ulipoangushwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Nchi za Magharibi kupitia NATO zilifanya uharibifu mkubwa na wa kiuadui wa miundombinu ya Libya na halafu ziliitelekeza nchi hiyo baada ya kulivunja jeshi lake, wakiacha kwa makusudi silaha zikiwa zimezagaa kwenye mikononi mwa makundi mbalimbali hasimu. Mbali na kusababisha ukosefu mkubwa wa usalama, hali hiyo imepelekea pia wahamiaji wengi, hasa kutoka barani Afrika, kujaribu kuvuka baharini kuelekea Ulaya kupitia Libya kutokana na kutokuweko serikali kuu yenye nguvu nchini humo.