Viongozi wa Umoja wa Afrika wakusanyika kwa mkutano muhimu Ethiopia
Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika umeanza leo Jumamosi katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ukiwakutanisha pamoja viongozi wa mataifa kujadili masuala muhimu ya kikanda na bara, ikiwemo amani na usalama, ujumuishaji wa kiuchumi, na mageuzi ya kitaasisi.
Katika mkutano huo wa siku mbili viongozi wa Afrika wanajadili hali ya amani na usalama, Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika, mageuzi ya kitaasisi katika jumuiya hiyo na masuala mengine ya kimkakati. Uchaguzi wa mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika pia unatarajiwa kufanyika.
Mgombea kutoka Kenya, Raila Odinga, anawania kuwa mrithi wa Moussa Faki Mahamat kama Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC)
Uchaguzi huo unafanyika leo Februari 15, katika kikao cha Marais ambacho kinatarajiwa kukamilika Jumapili Februari 16. Waziri huyo mkuu wa zamani wa Kenya mwenye umri wa miaka 80 anaingia kwenye kinyang'anyiro kikali dhidi ya Mahmoud Ali Yousuf wa Djibouti na Richad Randrimandrato wa Madagascar.
Mkutano huo pia utashughulikia nafasi inayokua ya Afrika katika mfumo wa kimataifa, na ripoti kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inatarajiwa pia kuwasilishwa.
Viongozi wa Afrika pia wanatarajiwa kuzindua juhudi mpya za fidia zinazohusiana na utumwa na ukoloni, na kaulimbiu ya mwaka huu, "Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia," ikilenga kushughulikia dhuluma za kihistoria na athari zake za kudumu barani Afrika.
Mpango huu unalenga kupata fidia za kifedha, kukiri rasmi makosa ya zamani, na mageuzi ya sera kutoka kwa mataifa ya kikoloni.
Mada nyingine muhimu katika mkutano wa leo wa AU ni mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Rais wa DRC Felix Tshisekedi hatashiriki mkutano huo lakini anawakilishwa na Waziri Mkuu, Judith Suminwa Tuluka.
Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, amechukua uenyekiti wa kuzunguka wa Umoja wa Afrika (AU) katika ufunguzi wa kikao cha leo.