Waziri Mkuu wa zamani wa Mauritius akamatwa kwa tuhuma za utakatishaji pesa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122826-waziri_mkuu_wa_zamani_wa_mauritius_akamatwa_kwa_tuhuma_za_utakatishaji_pesa
Waziri Mkuu wa zamani wa Mauritius Pravind Jugnauth amekamatwa na anakabiliwa na shtaka la utakatishaji pesa. Hayo yameelezwa na Tume ya Uhalifu wa Kifedha inayoendeshwa na serikali ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 16, 2025 23:37 UTC
  • Pravind Jugnauth
    Pravind Jugnauth

Waziri Mkuu wa zamani wa Mauritius Pravind Jugnauth amekamatwa na anakabiliwa na shtaka la utakatishaji pesa. Hayo yameelezwa na Tume ya Uhalifu wa Kifedha inayoendeshwa na serikali ya nchi hiyo.

Taarifa ya tume hiyo imesema, Jugnauth amewekwa chini ya ulinzi kufuatia upekuzi wa makachero wa tume katika maeneo tofauti, yakiwemo makazi yake.
 
Msemaji wa Tume, Ibrahim Rossaye amesema, walikuta na kunasa pesa taslimu zenye thamani ya dola milioni 2.4 katika biashara anayohusishwa nayo waziri mkuu huyo wa zamani.
 
Wakili wa Jugnauth alisema jana Jumapili kuwa mteja wake amefunguliwa mashtaka ya muda na ameyakana makosa aliyohusishwa nayo.
 
Pravind Jugnauth alikuwa waziri mkuu wa Mauritius kuanzia mwaka 2017 hadi Novemba mwaka jana wakati chama chake cha Vuguvugu la Wanamgambo wa Kisoshalisti kiliposhindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.
 
Kufuatia uchaguzi huo, Waziri Mkuu mpya Navin Ramgoolam alitangaza uamuzi wa kuzifanyia ukaguzi hesabu za fedha za umma.
 
Siku kadhaa zilizopita, Ramgoolam alitilia shaka usahihi wa taarifa fulani za serikali zilizokusanywa na utawala uliopita.
 
Mwezi uliopita, gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Mauritius naye pia alitiwa nguvuni kisha akaachiwa kwa dhamana baada ya kufunguliwa shtaka la kula njama ya kufanya udanganyifu.../