Maelfu ya Wakongo kutoka mashariki mwa nchi wakimbilia Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122856-maelfu_ya_wakongo_kutoka_mashariki_mwa_nchi_wakimbilia_burundi
Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbilia katika nchi jirani ya Burundi wakikimbia machafuko katika maeneo yao.
(last modified 2025-02-17T07:56:49+00:00 )
Feb 17, 2025 07:56 UTC
  • Maelfu ya Wakongo kutoka mashariki mwa nchi wakimbilia Burundi

Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbilia katika nchi jirani ya Burundi wakikimbia machafuko katika maeneo yao.

Waziri wa Burundi na chanzo cha misaada ya kibinadamu kimethibitisha siku ya Jumapili kuwasili kwa maelfu ya wakimbizi wa Kongo waliokimbia mapigano kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Martin Niteretse ameripoti kuwasili kwa "maelfu ya wakimbizi wa Kongo", lakini akasema idadi yao bado inatathminiwa. "Waliingiwa na hofu waliposikia kuwa jiji la Bukavu limechukuliwa na M23," Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Martin Niteretse ameziambia duru za habari.

"Tangu siku ya Ijumaa jioni, tumekuwa tukikabiliwa na ujio mkubwa wa wakimbizi wa Kongo," kimesema chanzo ndani ya shirika lisilo la kiserikali kiliyoko upande wa mpaka wa Burundi. "Kuna watu zaidi ya 10,000 na zaidi wameendelea kuwasili leo," kimeongea chanzo hiki.

Waasi wa M23 wamekuwa wakijaribu kuelekea kusini upande wa Bukavu, tangu walipouteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Kongo, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Hayo yanajiri katika halii ambayo, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, , amesema kuwa, Kinshasa inatafuta "njia za kukabiliana" na Rwanda kutokana na kuongezeka taharuki na mapigano mashariki mwa DRC.

Licha ya kuwa Rwanda inakana kuwaunga mkono waasi hao, lakini duru mbalimbali za kieneo na kimataifa zikiwemo ripoti za Umoja wa Mataifa zinasisitiza juu ya kupata himaya waasi hao kutoka Rwanda.