Serikali ya DRC yasema Jeshi la Rwanda limeingia Bukavu Mashariki
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imesema kuwa jeshi la Rwanda na washirika wake wameingia katika mji wa Bukavu, mashariki mwa nchi hiyo, katika jimbo la Kivu Kusini, na kuwataka wananchi kuwa macho.
Wizara ya Mawasiliano ya DRC imesema kupitia mtandao wa X kwamba: "Serikali inafuatilia hali inayoendelea Bukavu, kufuatia kuingia huko kwa jeshi la Rwanda na washirika wake."
Waasi wa M23 walidai siku ya Ijumaa kuwa wameuteka uwanja wa ndege wa Kavumu, ulioko kilomita 25 (maili 15) kutoka mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu. Aidha, waasi hao wameingia Bukavu baada ya kuteka Kavumu.
Serikali ya DRC imelaani kupuuzwa kwa suluhisho la amani na imeitaka jamii ya kimataifa kusaidia kusimamisha mapigano.
Taarifa ya Wizara ya Mawasiliano ya DRC imesema: "Rwanda inasisitiza mpango wake wa kukalia kwa mabavu ardhi, kupora mali na kufanya uhalifu pamoja na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika ardhi yetu."

Serikali imewahakikishia wananchi kuwa inafanya "kila linalowezekana kurejesha utulivu, usalama, na uhuru wa ardhi ya taifa," huku ikiwasihi wananchi "kusalia majumbani na kuepuka kujitokeza hadharani ili wasiwe shabaha ya vikosi vya uvamizi."
Kulingana na serikali ya Kongo miji ya Bukavu, Goma, na maeneo mengine yote yanayokaliwa kwa mabavu katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambayo yamekumbwa na uasi wa muda mrefu, ni "nembo ya mapabano"
Tangu Januari 26, watu zaidi ya 3,000 wameuawa, 2,880 wamejeruhiwa, na zaidi ya 500,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku wakiongeza idadi ya wakimbizi wa ndani ambao tayari wamefikia milioni 6.4, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Kwa uchache walinda amani 20, wakiwemo 14 kutoka Afrika Kusini, wameuawa hivi karibuni katika mapigano kati ya waasi wa M23 na majeshi ya Kongo.
Kinshasa inailaumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na kutuma majeshi mashariki mwa Kongo tangu mashambulizi ya hivi karibuni yalipoanza. Hata hivyo, Kigali imekana mara kwa mara madai hayo kwamba inawaunga mkono waasi.