Hamas yasifu msimamo wa viongozi wa Afrika dhidi ya Israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina , Hamas, imesifu msimamo wa "kiadilifu na jasiri" wa viongozi wa Afrika kuhusu mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, pamoja na upinzani wao mkali dhidi ya kampeni ya kikatili inayoendelea dhidi ya Wapalestina.
Katika Mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, siku ya Jumapili, viongozi wa AU walitoa taarifa kali ya kulaani ukatili wa Israel katika Ukanda wa Gaza, wakihimiza nchi wanachama kusitisha ushirikiano na hatua za kuwa na mahusiano ya kawaida na utawala haramu wa Israel.
"Tunalaani vikali mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina na tunataka hatua za kimataifa zichukuliwe dhidi ya vitendo hivi," ilisomeka taarifa ya mwisho ya mkutano huo.
Aidha viongozi hao wa Afrika wamesema: “Tunatoa wito wa kukomesha ushirikiano na uhusiano wa kawaida na Israel hadi itakapositisha uvamizi wake na ukandamizaji dhidi ya Palestina."
Hamas, katika tamko lake, imesema kuwa inapongeza taarifa ya mwisho ya mkutano wa Umoja wa Afrika na msimamo wa kiadilifu na wa kishujaa wa nchi wanachama katika kulaani vita vya kikatili vya Wazayuni dhidi ya Gaza, pamoja na kukataa ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala huo.
Harakati hiyo yenye makao yake Gaza imelisifu tamko hilo kwa kulaani mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kutoa wito wa kushtakiwa utawala wa Kizayuni katika mahakama za kimataifa, pamoja na kusitishwa aina zote za ushirikiano na mahusiano ya kawaida na utawala huo wa kikoloni hadi utakapoachana na uvamizi wake dhidi ya Wapalestina.
Hamas imeeleza kuwa msimamo wa mataifa ya Afrika ni mwendelezo wa kihistoria wa mapambano ya bara hilo dhidi ya ukoloni na uonevu, pamoja na kushikamana kwao na thamani za uhuru, uadilifu na haki ya kujiamulia hatma yao.
Harakati hiyo imesisitiza kuwa msimamo huo thabiti unadhihirisha uungaji mkono kwa uthabiti wa Wapalestina dhidi ya jinai za utawala wa kikoloni wa Israel, na kutuma ujumbe wazi kwa jamii ya kimataifa kwamba inapasa kutimiza wajibu wake wa kusitisha uchokozi wa Wazayuni na kuwashtaki viongozi watenda jinai wa Israel.
Mwishowe, Hamas imetoa wito kwa mataifa ya Afrika kuchukua hatua madhubuti kwa kuongeza mashinikizo ya kisiasa na kisheria dhidi ya Israel, kuunga mkono suala la Palestina katika majukwaa ya kimataifa na kuimarisha uthabiti wa Wapalestina hadi uhuru kamili upatikane na taifa huru la Palestina liundwe huku al-Quds (Jerusalem) ukiwa mji mkuu wake.