Afrika Kusini yapata msaada kutoka China baada ya vikwazo vya Trump
-
Ronald Lamola
Marekani haikujibu maombi ya Afrika Kusini ya kujadili kupunguzwa kwa misaada ya Rais wa Marekani Donald Trump, na kufuatia jambo hilo China imeahidi kuipa Pretoria msaada unaohitajika.
Hayo yamedokezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, ambaye ameongeza kuwa nchi yake inafanya mazingumzo na nchi kadhaa ikiwemo China, ambayo imeonyesha mshikamano na kutangaza kuwa tayari kutoa msaada katika mahusiano ya kibiashara.
Lamola ameongeza kuwa, Marekani pia imepinga mada ya mkutano wa nchi zilizoendelea za G20 ambayo ni "Mshikamano, Usawa, Uendelevu." Lamola amesema kuwa ajenda ya mkutano ujao wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 huko Johannesburg itabaki bila kubadilika na kwamba ombi la Marekani limepuuzwa, kwani nchi za G20 tayari ziliafikiana kuhusu mada hiyo.
Lamola amesisitiza kuwa sera ya marekebisho ya ardhi ya Afrika Kusini na kesi yake ya mauaji ya kimbari katika ICJ dhidi ya Israel "haiwezi kujadiliwa."
Trump amefuta misaada kwa Afrika Kusini kutokana na nukta hizo mbili lakini wakuu wa nchi hiyo wamesisitiza kuwa hawatalegeza msimamo.