UNHCR: Karibu wakimbizi 15,000 kutoka DRC wameingia Burundi
Zaidi ya watu 10,000 hadi 15,000 wamevuka mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kuingia Burundi katika siku chache zilizopita wakikimbia mapigano yanayoshadidi mashariki mwa DRC.
Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi, Matthew Saltmarsh amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumanne kuwa idadi kubwa ya waliowasili ni raia wa DRC, hasa kutoka eneo la Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini, ambako hali ya usalama inazidi kuzorota. Aidha amesema kuna idadi ndogo ya raia wa Burundi ambao wameamua kurejea nchini mwao wakikimbia mapigano.
Amesema wanaingia kupitia kituo cha mpakani cha Gatumba kilicho karibu na jiji kubwa la Burundi, Bujumbura, wakiwa wamechoka na msongo wa mawazo, huku wengi wakiwa wametengana na familia zao bila taarifa zozote juu ya waliko wapendwa wao.
Ripoti zinaonesha kuwa maelfu ya watu wanavuka kupitia njia zisizo rasmi, ikiwemo mto Rusizi karibu na Rugombo, huku kukiwa na taarifa za watu kadhaa kuzama maji.
Hali katika jamii zilizo karibu na mpaka ni mbaya sana, kukiwa na uhaba wa makazi, maji safi na huduma za afya. Katika eneo moja, watu wapatao 10,400 wanahifadhiwa katika shule na uwanja wa michezo upande wa DRC wakisubiri kuhamishiwa maeneo salama zaidi.
Waasi wa M23 wameteka miji mikubwa ya Bukavu na Goma, mashariki mwa DRC katika kipindi cha mwezi moja uliopita.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amesema kuwa, Kinshasa inatafuta "njia za kukabiliana" na Rwanda kutokana na kuongezeka taharuki na mapigano mashariki mwa DRC.
Licha ya kuwa Rwanda inakana kuwaunga mkono waasi hao, lakini duru mbalimbali za kieneo na kimataifa, zikiwemo ripoti za Umoja wa Mataifa, zinasisitiza kuwa waasi hao wanapata himaya kutoka Rwanda.