Waasi wa Tuareg: Jeshi la Mali limewaua raia 24 kaskazini mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122930-waasi_wa_tuareg_jeshi_la_mali_limewaua_raia_24_kaskazini_mwa_nchi
Muungano wa waasi wa Tuareg huko kaskazini mwa Mali umewatuhumu wanajeshi wa nchi hiyo kwa kuwaua raia 24 waliokuwa wakisafiri kuelekea kaskazini mwa Algeria kutoka mji wa Gao, huku jeshi likiripoti habari ya kujiri mapigano katika eneo hilo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 19, 2025 08:33 UTC
  • Waasi wa Tuareg: Jeshi la Mali limewaua raia 24 kaskazini mwa nchi

Muungano wa waasi wa Tuareg huko kaskazini mwa Mali umewatuhumu wanajeshi wa nchi hiyo kwa kuwaua raia 24 waliokuwa wakisafiri kuelekea kaskazini mwa Algeria kutoka mji wa Gao, huku jeshi likiripoti habari ya kujiri mapigano katika eneo hilo.

Mali, inayoongozwa na serikali ya kijeshi, kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, imekuwa ikipigana na makundi ya wanamgambo yanayoshirikiana na ISIS (Daesh) na al Qaeda, huku ikikabiliana pia na historia ndefu zaidi ya uasi unaoongozwa na waasi wa Tuareg kaskazini mwa nchi.

Chama cha Ukombozi cha Azawad (FLA) kimesema raia hao walikuwa wakisafiri kwa magari mawili, na kwamba moja lilichomwa moto huku jingine likikimbia na baadhi ya watu walionusurika.

Familia za wahanga pamoja na msemaji wa jumuiya ya haki za binadamu ya eneo hilo ya Kal Akal, wamethibitisha habari ya tukio hilo katika mahojiano na Reuters.

Wapiganaji wa Tuareg

Habari zaidi zinasema kuwa, moja ya magari hayo, lilikuwa likisafirisha wahamiaji, jamaa za dereva wamesema.

Haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya Mali kutangaza kuwa, itaanza kuwajumuisha wapiganaji 2,000 kutoka makundi washirika yenye silaha katika jeshi na vikosi vya usalama, kwa lengo la kujenga amani na harakati mbalimbali ambazo zimekuwa zikipigana dhidi ya serikali.