Uganda yasema imeweza kudhibiti mlipuko wa Ebola
Uganda imesema imeweza "kudhibiti" mlipuko wa hivi karibuni wa virusi vya Ebola aina ya Sudan, ambao ulithibitishwa na Wizara ya Afya mwishoni mwa Januari.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki iliwaruhusu wagonjwa wote wanane wa Ebola kuondoka hospitalini Jumanne baada ya kupimwa na kuthibitika kuwa hawana virusi hivyo, na hakuna vifo vipya vilivyoripotiwa kutokana na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Jane Aceng, amesisitiza kuwa ingawa nchi hiyo imeweza kudhibiti ugonjwa huo, mlipuko huo bado haujatangazwa kuwa umemalizika.
Kulingana na Aceng, Takriban watu 265 waliotangamana na wagonjwa, ambao hawajaonyesha dalili za Ebola aina ya Sudan, bado wako chini ya karantini na wanaendelea kufuatiliwa,.
Kampala ilithibitisha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola wa virusi vya Sudan (SVD) mnamo Januari 30, baada ya mgonjwa wa kwanza aliyerekodiwa, muuguzi wa miaka 32, kufariki kutokana na ugonjwa huo. Tangu wakati huo, visa vingine vinane vimekuwa vikitangazwa.
Uganda imeripoti milipuko sita ya SVD katika miaka ya 2000, 2011, 2012, 2022, na 2025, ikiwemo mlipuko wa hivi karibuni. Mlipuko wa awali mwishoni mwa 2022 ulisababisha vifo vya watu 55.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Ebola ya Sudan ni mojawapo ya aina sita za virusi vya Ebola. Hakuna chanjo iliyoidhinishwa dhidi ya virusi vya Ebola ya Sudan. Hata hivyo, majaribio ya kitabibu ya chanjo inayoweza kuwa na ufanisi dhidi ya ugonjwa huo yalianza baada ya WHO kutoa dozi 2,160 za chanjo ya majaribio na matibabu kwa Uganda.