Maafisa wa Afrika wa Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu mzozo wa DRC
Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa barani Afrika wametahadharisha kuhusu mzozo na machafuko yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Maafisa hao wanasema kuwa, mashambulizi ya waasi wa M23 mashariki mwa DRC yanatishia amani ya eneo zima.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Bintu Keita amesema kuwa, ni muhimu kwa Baraza la Usalama kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kuepusha vita vya kikanda.
Kwa upande wake Huang Xia mjumbe maalumu wa Ukanda wa Maziwa Makuu kwenye umoja huo amesema kuwa, hatua ya waasi wa M23 ya kuidhibiti miji mikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kunaashiria kitisho kinachoukabili ukanda huo kuliko awali.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, jana (Jumatano) milio ya risasi ilisikika katika mji wa Uvira, mji ulio kwenye mpaka na Burundi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Duru za ndani zimesema hayo wakati mapigano yakizuka kati ya vikosi vya serikali na washirika huku waasi wanaoaminika kuungwa mkono na Rwanda wakisonga mbele.
Wakazi na maofisa wameeleza matukio ya uporaji, maiti zikiwa mitaani na askari wa serikali wakijaribu kutumia boti kutoroka kupitia Ziwa Tanganyika. Wafungwa katika jela ya Uvira wametoroka.
Zaidi ya watu 10,000 hadi 15,000 wamevuka mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kuingia Burundi katika siku chache zilizopita wakikimbia mapigano yanayoshadidi mashariki mwa DRC.
Licha ya kuwa Rwanda inakana kuwaunga mkono waasi hao, lakini duru mbalimbali za kieneo na kimataifa, zikiwemo ripoti za Umoja wa Mataifa, zinasisitiza kuwa waasi hao wanapata himaya kutoka Rwanda.