Umoja wa Mataifa waonya dhidi ya kutangazwa serikali nyingine nchini Sudan
-
Stephane Dujarric
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba tangazo la serikali nyingine nchini Sudan linatishia "kuzidisha mgogoro" unaoendelea nchini humo.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameeleza wasiwasi wake kuhusu tangazo lililopangwa kutolewa kesho Ijumaa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) la kuundwa serikali nyingine, jambo ambalo amesema litazidisha "mgawanyiko" na "mgogoro" nchini Sudan.
Stephane Dujarric amesema: "Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka zaidi mzozo nchini Sudan, na hatua yoyote kama hiyo itaigawa zaidi nchi hiyo na kuzidisha mgogoro."
Dujarric amesisitiza kuwa "kulinda umoja, mamlaka na ardhi nzima ya Sudan bado ni nguzo muhimu katika njia ya kupatikana suluhisho la kudumu la mzozo huo na kufikia utulivu wa muda mrefu kwa nchi na kanda nzima."
Kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) ambalo limekuwa vitani na jeshi la Sudan kwa karibu miaka miwili, limetangaza kwamba linakaribia kusaini "mkataba wa kuanzisha serikali ya amani na umoja nchini Sudan."
Hafla ya tangazo hilo, ambayo awali ilipangwa kufanyika Jumanne iliyopita katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta nchini Kenya, iliahirishwa hadi kesho Ijumaa, huku kukiwa na mgawanyiko kati ya makundi yanayoshirikiana na RSF.
Serikali ya Sudan siku ya Jumanne ililaani kitendo cha Kenya kuandaa mkutano uliojumuisha makundi ya kisiasa ya upinzani na viongozi wa kundi la waasi la RSF kwa lengo la kuunda serikali nyingine, na kutangaza kuwa hatua hiyo "inahamasisha kugawanywa nchi za Kiafrika na ni kielelezo cha kupuuza kanuni za ujirani mwema."