Wasudan wanarejea makwao licha ya kuandamwa na mashaka na matatizo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i122996-wasudan_wanarejea_makwao_licha_ya_kuandamwa_na_mashaka_na_matatizo
Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Sudan wameendelea kurejea katika maeneo yao waliyoyakimbia kutokana na vita, lakini bado hofu na wasiwasi umetamalaki kwenye nyoyo zao.
(last modified 2025-02-20T22:56:05+00:00 )
Feb 20, 2025 22:56 UTC
  • Wasudan wanarejea makwao licha ya kuandamwa na mashaka na matatizo

Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Sudan wameendelea kurejea katika maeneo yao waliyoyakimbia kutokana na vita, lakini bado hofu na wasiwasi umetamalaki kwenye nyoyo zao.

Miongoni mwao ni Bi Enas El-Tom, 37, ambaye huku akiwa na hisia tofauti za furaha na hofu, alipanda basi na watoto wake watatu, wakaanza safari ya kurejea nyumbani kwake Wad Madani, makao makuu ya Jimbo la Gezira katikati mwa Sudan, baada ya kupitisha karibu mwaka mmoja katika kambi ya wakimbizi huko Port Sudan ya Jimbo la Bahari Nyekundu. Wakimbizi mbalimbali waliohojiwa na vyombo vya habari wamesema kuwa wana hisia mchanganyiko, lakini nyumbani ni nyumbani, kuwezi kupafananisha na sehemu nyingine yoyote.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Februari, mamlaka za Jimbo la Bahari Nyekundu huko Sudan zimekuwa zikiandaa safari za kurejea kwa hiari watu waliokimbia makazi yao katikati mwa Sudan baada ya jeshi la nchi hiyo SAF kuutwaa tena mji wa Wad Madani Januari 11, 2025.

El-Tom ambaye ni mjane mwenye watoto watatu amenukuliwa akisema: "Hisia zangu zimechanganyika -- nimefarijika kurejea nyumbani na kusalimika na ugumu wa maisha katika kambi ya wakimbizi, lakini ninahofia kutojulikana muustakbali wetu. Hatujui iwapo hali ni salama huko Wad Madani au la. Hatujui hali hiyo itaendelea hadi lini. Pia tuna wasiwasi kuhusu ukosefu wa huduma za kimsingi."

Amma katika kituo cha basi huko Port Sudan, mkimbizi mwingine Bi Halima Ismail amehojiwa akiwa amesimama karibu na basi na kusema kuwa, anaamini kwamba kurejea nyumbani kutakuwa suluhisho bora kwa baba yake, ambaye ameugua ugonjwa wa moyo kwa zaidi ya miaka 20.