Rais wa Afrika Kusini amwalika mwenzake wa Ukraine kwa ziara ya kiserikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i123038-rais_wa_afrika_kusini_amwalika_mwenzake_wa_ukraine_kwa_ziara_ya_kiserikali
Rais Cyril Ramaphos wa Afrika Kusini amemwalika rais mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky afanye ziara ya kiserikali nchini humo.
(last modified 2025-02-21T23:39:39+00:00 )
Feb 21, 2025 23:39 UTC
  • Rais wa Afrika Kusini amwalika mwenzake wa Ukraine kwa ziara ya kiserikali

Rais Cyril Ramaphos wa Afrika Kusini amemwalika rais mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky afanye ziara ya kiserikali nchini humo.

Rais Ramaphosa amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa, kwamba Afrika Kusini itaendeleza kuwa na msimamo wake wa kuunga mkono mchakato wa mazungumzo kati ya Russia na Ukraine.

Amesema: "Ninakaribisha ushirikiano mzuri niliokuwa nao na Rais Zelensky na ninatarajia kumpokea nchini Afrika Kusini hivi karibuni kwa ziara ya kiserikali."

Kwa upande wake, Vincent Magwenya, msemaji wa rais wa Afrika Kusini amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, tarehe hasa ya ziara hiyo bado haijathibitishwa.

Zelensky kwa upande wake amemshukuru Ramaphosa kwa kuunga mkono kile alichokiita "uhuru wa Ukraine na uadilifu wa kieneo" na ameelezea matumaini yake ya kupatikana amani ya kudumu mwaka huu.

Zelensky amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa: "Lililo muhimu ni kwamba nchi zetu zina msimamo sawa; hakuna chochote kinachowezekana Ukraine bila ya kuwepo Ukraine yenyewe. Sote tuna matumani ya kufikia amani ya haki na ya kudumu mwaka huu. Sauti ya Afrika Kusini ni muhimu na tunategemea uungaji mkono wake."

Afrika Kusini imekuwa na msimamo wa kutoegemea upande wowote katika mzozo wa Russia na Ukraine na muda wote imekuwa ikizitaka nchi hizo mbili kutatua matatizo yao kwa njia ya mazungumzo.