Wakimbizi zaidi waendelea kumiminika nchini Burundi
Idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini Burundi kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inazidi kuongezeka huku juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa mashariki mwa DRC zikiwa bado hazijazaa matunda.
Mwakilishi wa shirika la kuhudumia wakimbizi wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi Brigitte Mukanga-eno, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba, mapema wiki hii zaidi ya watu elfu 9 walivuka mpaka kutoka DRC na kuingia Burundi.
Maeneo kadhaa kaskazini magharibi mwa Burundi watu wamejaa wengine wamekoseshwa makazi mara kadhaa na wamewasili wakiwa wamejeruhiwa au wana matatizo ya afya kama vile Surua, hiyo ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) linatarajia kuwahamisha watu waliokoseshwa makazi ambao wamehifadhiwa kwa muda katika uwanja wa michezo ulio wazi pamoja na shule na makanisa katika eneo la ardhi ambalo huduma za kibinadamu zinaweza kutolewa.
NHCR imetoa ombi la dola milioni 40.4 ili kujiandaa na kutoa huduma za kuokoa maisha na usaidizi kwa wakimbizi wa ndani na waliokimbilia nchi jirani baada ya wakati huu ambapo mashambulizi ya waasi wa M23 yanazidi kufurusha raia.
Taarifa ya UNHCR inasema tangu Januari 26 mwaka huu M23 walipoingia Goma, jimboni Kivu Kaskazini, wameendelea na mashambulizi na kutwaa miji sio tu Goma, bali pia Kamanyola na Bukavu jimboni Kivu Kusini.